Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imeelekeza mazingira kuwa sehemu ya lazima katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na maendeleo ya miji nchini, ikisisitiza kuwa ukuaji wa makazi unapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maelekezo hayo yametolewa na Makamu wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Juni 5, 2026 jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa mamlaka zote za serikali, taasisi na wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Nchimbi amesema Serikali imeamua kuimarisha usimamizi wa mazingira kwa kuhusisha hatua za kijani katika shughuli za maendeleo, ikiwemo kuweka sharti la kupanda angalau miti mitano kwa kila kibali kipya cha ujenzi kitakachotolewa.
Aidha, amesema Manispaa na Majiji yote nchini yanapaswa kuhakikisha miji inakuwa na bustani za kijani zinazotunzwa ipasavyo ili kuboresha mazingira ya makazi na kupunguza athari za ongezeko la joto duniani.
Katika hatua nyingine, ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha upatikanaji wa miche ya miti ya kutosha ili kuwezesha utekelezaji wa kampeni za upandaji miti nchini, huku Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zikihakikisha misitu inayostahili inasajiliwa kwa ajili ya kuhifadhi hewa ukaa.
Pia, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetakiwa kuimarisha usimamizi wa mipango miji ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaotokana na ukuaji holela wa makazi.
Dk. Nchimbi amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuongezeka duniani, hivyo Tanzania inapaswa kuchukua hatua za haraka na za pamoja ili kulinda rasilimali za asili na kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu.
“Tunapaswa kuchukua hatua sasa kwa sababu mazingira ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji majibu ya pamoja kutoka kwa kila sekta,” amesema.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema Serikali imezindua Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania itakayoratibu ushirikiano wa wadau mbalimbali katika juhudi za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema programu hiyo itashirikisha taasisi za umma, sekta binafsi, mashirika na wananchi ili kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.




Social Plugin