Na, mwandishi wetu - Arusha
SERIKALI imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya uadilifu katika utumishi wa umma ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu na mipango ya maendeleo unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Hayo yamesemwa hii leo (12 Juni, 2026) na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati akifungua Mafunzo ya Kamati ya Uadilifu yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati Maalum ya Menejimenti katika kusimamia masuala ya uadilifu katika ofisi hiyo.
“Uadilifu ni nguzo muhimu katika ufanikishaji wa majukumu na utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika sehemu za kazi,” amesema Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi amesema kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuhakikisha anazingatia maadili ya kazi na kulinda misingi ya uadilifu ili kuimarisha utendaji na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali.
Aidha, Dkt. Yonazi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wajumbe kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Uadilifu kwa kuhakikisha unaingizwa katika mipango kazi na bajeti za mwaka za taasisi.
Vilevile, amebainisha kuwa Kamati za Uadilifu zina jukumu la kusimamia utekelezaji wa sera dhidi ya rushwa na kuhakikisha watumishi wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Kuna umuhimu wa kuimarisha uwazi na uwajibikaji pamoja na kuanzisha mifumo madhubuti ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia usiri.
Akiwasilisha mada ya masuala ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP IV) 2023-2030 Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais Ikulu Bw. Andrew Massawe amesema, ni wajibu wa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na kupinga vitendo vyote vinavyoashiria mazingira ya rushwa ili kuendelea kuhudumia wananchi, na Taifa kwa ujumla katika misingi sahihi ya utumishi wa umma.
“Tufanye kazi kwa uadilifu na kuzingatia masuala ya huduma bora kwa wateja, tusihudumie watu kama favor bali tutoe huduma kwa viwango bora vinavyotakiwa,”alisema Bw. Massawe




Social Plugin