Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katika kuendeleza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kukuza ubunifu na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, washiriki 100 bora wamechaguliwa kuendelea na hatua inayofuata ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026 baada ya ushindani mkubwa ulioshirikisha maombi 7,852 kutoka mikoa yote ya Tanzania.
Akizungumza jijini Dodoma June 4,2026 Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga, amesema shindano hilo lenye kaulimbiu “Wanafikiri, Taifa Linasonga” limebeba dhamira ya kuibua mawazo bunifu ya vijana yatakayochangia kuimarisha uchumi wa Tanzania, kukabiliana na athari za misukosuko ya kiuchumi duniani na kuunga mkono utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema mwitikio wa vijana umekuwa wa kuvutia, ambapo sekta ya TEHAMA na huduma za kidigitali imeongoza kwa asilimia 30.7 ya mawazo yaliyowasilishwa, ikifuatiwa na kilimo na teknolojia za kilimo kwa asilimia 27.8, huku sekta ya viwanda na uzalishaji ikichangia asilimia 21.3 ya mawazo yote yaliyopokelewa.
Kwa mujibu wa Sanga, uchambuzi wa awali ulionesha kuwa maombi 4,121 sawa na asilimia 52.5 yalitimiza vigezo vya msingi vya ushiriki, huku mawazo 458 yakifanikiwa kufika katika hatua ya mwisho ya tathmini kabla ya kupatikana washiriki 100 bora waliotangazwa rasmi.
Amefafanua kuwa washiriki hao wamechaguliwa kwa kuzingatia ubora wa mawazo yao, kiwango cha ubunifu, uwezekano wa kuyatekeleza na mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa, akibainisha kuwa kufika hatua hiyo ni mafanikio makubwa kutokana na ushindani mkali uliokuwepo.
Aidha, washiriki hao wataingia katika kambi maalum ya mafunzo ya siku nne watakayopatiwa mafunzo ya kitaalamu na ushauri wa kuboresha mawazo yao kabla ya kufanya mawasilisho yatakayochuja washiriki 30 bora wa nusu fainali na baadaye 10 bora watakaoingia hatua ya fainali.
Sanga ameongeza kuwa kutokana na mwitikio mkubwa na ubora wa mawazo yaliyowasilishwa, waandaaji wameongeza thamani ya zawadi ambapo mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi milioni 50, mshindi wa pili milioni 30 na mshindi wa tatu milioni 20.
Mbali na zawadi hizo, washiriki wote 100 bora watapatiwa vyeti vya utambuzi pamoja na fursa za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kuunganishwa na wadau mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa mawazo yao kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa na uchumi wa nchi.



Social Plugin