Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PSSSF YAASA WABUNGE KUIFANYA SEKTA YA NGOZI KUWA MWAMBA WA VIWANDA NA AJIRA NCHINI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Katika harakati za kukuza uchumi wa viwanda nchini, Mfuko
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umehimiza Wabunge kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ngozi zinazozalishwa ndani ya Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kukuza thamani ya rasilimali za taifa.

Akizungumza Juni 15, 2026 katika Ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Fortunatus Makore Magambo alieleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kujenga uchumi imara kupitia sekta ya ngozi, endapo bidhaa zake zitapata soko la kutosha la ndani na nje ya nchi.

Akiwasilisha taarifa ya shughuli na mafanikio ya Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited (KLICL), Magambo alisema uwekezaji uliofanyika katika sekta hiyo tayari umeanza kuleta matokeo chanya kwa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kuimarisha mnyororo wa uzalishaji wa viwanda.

Amesema sekta ya ngozi ni miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuchochea ajira kwa vijana, hasa kupitia uzalishaji wa bidhaa kama viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya kimataifa.

“Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muwe mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini. Mkitumia na kuzitangaza mtasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuongeza soko la bidhaa zetu za ndani,” amesema Magambo.

Kwa mujibu wake, KLICL imeweka mikakati ya kupanua masoko yake ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha uwezo wake wa uzalishaji unatumika kikamilifu. Masoko lengwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki, China, Saudi Arabia, Italia, UAE, Misri, Pakistan na Uturuki.

Katika hatua inayoonesha kuimarika kwa ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa, wanunuzi kutoka China tayari wameidhinisha sampuli za bidhaa za kiwanda hicho, hatua inayofungua milango ya oda kubwa zaidi katika siku zijazo.

Aidha, kiwanda hicho kimefanikiwa kuuza vipande 48 vya ngozi ya mbuzi kwenda China kwa thamani ya dola za Marekani 15,000, ikiwa ni ishara ya mwanzo wa ukuaji wa soko la nje.

Hata hivyo, changamoto kubwa iliyobainishwa ni upanuzi wa masoko kuendana na uwezo wa uzalishaji, ambapo Magambo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani.

Kwa ujumla, sekta ya ngozi nchini inaendelea kujidhihirisha kama moja ya nguzo muhimu za uchumi wa viwanda, ikiwa na uwezo wa kugeuza rasilimali za mifugo kuwa bidhaa zenye thamani kubwa na zinazoshindana kimataifa.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com