Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imeeleza dhamira yake ya kuimarisha mazingira ya kazi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini kupitia mwongozo mpya wa uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (NaCoNGO), hatua inayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wadau hao katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa NaCoNGO jijini Dodoma Leo June 25,2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk.Dorothy Gwajima, amesema mwongozo huo umeweka msingi imara wa ushirikiano wa kisasa kati ya Serikali na mashirika ya kiraia kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Amesema mwongozo huo unalenga kuyaunganisha mashirika hayo ili yawe na sauti moja katika kuwasilisha mawazo, mapendekezo na mchango wake kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Huu ni mwongozo unaoongeza nguvu ya mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuweka wazi misingi ya uwazi, uwajibikaji, uaminifu na namna ya kuepuka migongano ya maslahi katika uongozi na utendaji wake," amesema.
Gwajima amesisitiza kuwa mifumo ndiyo inapaswa kuongoza taasisi badala ya maamuzi yanayotegemea ukaribu wa watu au maslahi binafsi.
"Kujuana iwe mwiko,tunataka mfumo ufanye kazi,tunataka kumaliza ukiritimba uliopo na ikiwezekana tupewe taarifa za wanaozuia maendeleo ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao," amesema.
Katika kuonesha changamoto zinazokwamisha jitihada za maendeleo, Waziri huyo amesema bado kuna matukio ambapo mashirika au watu binafsi wanaojitolea kusaidia jamii hukumbana na vikwazo visivyo vya lazima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuondoa ukiritimba katika sekta binafsi ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na usajili wa kampuni ili kurahisisha uwekezaji na uanzishaji wa miradi mipya.
Waziri Gwajima pia aliwataka viongozi wa NaCoNGO kusimamia kwa karibu maadili ya taasisi hiyo na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kudhoofisha dhamira ya baraza hilo.
"Mjilinde wenyewe. Kwenye msafara wa mamba na kenge wapo. Hakikisheni uongozi wa NaCoNGO unalindwa na kuongozwa kwa misingi ya uwazi na uwajibikaji," amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kukuza haki za wananchi, ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa, hivyo itaendelea kuyashirikisha kama wadau muhimu wa maendeleo.
"Nyie ni wadau wetu, si washindani wetu. Tumekuwa tukiona mchango wenu mkubwa katika jamii na tutaendelea kuwasikiliza," amesema.
Katika hatua nyingine, alimuomba Katibu Mkuu wa Wizara kuhakikisha mashirika yanayofanya vizuri yanatambuliwa na kupewa motisha kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa katika mwongozo huo mpya.
Pia amependekeza mashirika yenye utendaji bora yawe yanapatiwa fursa ya kushiriki mikutano na majukwaa ya kimataifa kwa lengo la kuongeza uzoefu na kupanua mtandao wa ushirikiano wa maendeleo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eliakimu Maswi amewataka viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuimarisha mifumo ya kidijitali, kufungua majukwaa ya mawasiliano ya kisasa na kuboresha usimamizi wa taarifa na nyaraka.
Ametoa mfano wa mfadhili aliyekuwa tayari kujenga wodi katika eneo alikozaliwa kwa gharama zake mwenyewe lakini akakumbana na urasimu uliochelewesha utekelezaji wa mradi huo.
"Kuna wakati mtu anajitolea kujenga kwa fedha zake mwenyewe, lakini badala ya kupewa ushirikiano anawekewa vikwazo. Hela hutafuti wewe, kwa nini ulete vizuizi? Tunapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi," amesema.
Amesema mwongozo huo ni mali ya umma na unapaswa kusomwa, kujadiliwa na kueleweka kwa wadau mbalimbali ili kuondoa dhana kwamba kuanzisha au kuendesha shirika lisilo la kiserikali ni jambo gumu.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira salama na rafiki yatakayowezesha mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa uhuru, uwazi na ufanisi kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa.






Social Plugin