Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BILIONI 51 ZIMETUMIKA KUBORESHA UWANJA WA NDEGE KIGOMA – PROF. MBARAWA




Na mwandishi wetu,Kigoma

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa  amesema Serikali imetumia shilingi bilioni 51 kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikia asilimia 67 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba au Novemba 2026

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Kigoma, leo tarehe 25 Juni, 2026 Prof. Mbarawa amesema jengo jipya la abiria litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria laki nne kwa mwaka na kupokea abiria 500 kwa wakati mmoja, hatua itakayoongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa anga katika ukanda huo

Ameongeza kuwa mradi huo utaiwezesha Kigoma kuwa na uwanja wa ndege wenye uwezo wa kutoa huduma mchana na usiku kutokana na uwekaji wa mifumo ya taa za kuongozea ndege

Aidha, amesema Serikali ina mpango wa kuongeza urefu wa njia ya kurukia na kutua ndege ili kuruhusu ndege kubwa zaidi kutumia uwanja huo

Prof. Mbarawa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kukamilika kwa mradi huo ambao ulikuwa umekwama kwa muda mrefu na kubainisha kuwa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Tabora na Sumbawanga tayari vimekamilika

Kwa upande wake, Meneja wa Viwanja vya Ndege Kanda ya Magharibi, Fadhili Magenema, amesema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) itaendelea kusimamia ukamilishaji wa mradi huo na kuboresha huduma za viwanja vya ndege nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com