Na mwandishi wetu
Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Hemed Jalala Mwakindenge, amesema Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448H unapaswa kuwa fursa muhimu kwa Watanzania kujitathmini binafsi na kitaifa, huku wakidumisha umoja, mshikamano na uvumilivu katika jamii.
Akitoa salamu za Mwaka Mpya wa Kiislamu, Sheikh Mwakindenge alisema kipindi hicho ni wakati mwafaka wa kutafakari mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza, ili kujenga msingi imara wa maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa amani na utulivu uliopo nchini ni tunu muhimu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania bila kujali tofauti za kidini, kisiasa au kijamii.
“Watanzania wanapaswa kuendelea kulinda amani, kupendana na kushikamana ili taifa letu liendelee kuwa mfano wa utulivu na maendeleo,” alisema Sheikh Mwakindenge.
Aidha, aliwataka wananchi kuendeleza maadili mema, kuheshimiana na kuvumiliana, akieleza kuwa mshikamano wa kitaifa ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.
Sheikh Mwakindenge pia alitoa wito kwa viongozi na wananchi kushirikiana katika kudumisha amani na maelewano, ili Tanzania iendelee kuwa kielelezo cha utulivu na mshikamano katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.
Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448H unawakumbusha waumini wa dini ya Kiislamu kuhusu tukio la Hijra ya Mtume Muhammad (S.A.W), ambalo linafundisha uvumilivu, kujitolea na umuhimu wa kujenga jamii yenye mshikamano na maadili mema.

Social Plugin