SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuonesha ubora wa huduma zake kwa wananchi kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, huku mamia ya wananchi na wafanyabiashara wakifurika katika banda la taasisi hiyo kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa njia ya kisasa.
Hayo yamesemwa leo Juni 23,2026 na Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Hamisi Sudi Mwanasala, amesema mwitikio wa wananchi katika maonesho hayo umekuwa mkubwa kutokana na hamu ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu viwango, ubora wa bidhaa na taratibu za usajili.
Amesema TBS imetumia maonesho hayo kama jukwaa la kuwasogezea wananchi huduma muhimu zikiwemo utoaji wa vibali, usajili wa bidhaa na majengo ya biashara ya chakula na vipodozi pamoja na kupokea maombi ya leseni ya kutumia Nembo ya Ubora ya TBS.
"Tumeshuhudia mwamko mkubwa wa wananchi. Wengi wamekuja na maswali mbalimbali kuhusu huduma zetu na wamepata majibu ya kina. Kiu yao ya kupata taarifa sahihi imeweza kutimizwa kupitia wataalamu waliopo katika banda letu," amesema Mwanasala.
Amefafanua kuwa pamoja na kutoa huduma, TBS imeendelea kutoa elimu kwa wazalishaji, wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa, kuingizwa au kuuzwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mwanasala, maonesho ya mwaka huu yamekuwa na umuhimu wa kipekee kwa TBS kwani yanafanyika wakati Shirika hilo likiadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, safari ambayo imeambatana na mafanikio makubwa katika kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma nchini.
Amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali, taasisi za umma na wananchi wa kawaida ambao wametoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha zaidi huduma za Shirika hilo.
Katika hatua nyingine, Mwanasala amesema TBS imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali kwa kuweka mifumo inayorahisisha upatikanaji wa huduma bila wananchi kusafiri umbali mrefu kufika kwenye ofisi za Shirika hilo.
Ametaja mifumo hiyo kuwa ni Online Application System (OAS) pamoja na Integrated Standardization, Quality Assurance, Metrology and Testing System (ISQMT), ambayo inamwezesha mteja kufanya maombi ya usajili wa bidhaa, usajili wa maeneo ya biashara ya vipodozi na chakula na kupata leseni ya kutumia Nembo ya Ubora kwa njia ya mtandao.
"Leo hii mteja anaweza kuwasilisha maombi yake akiwa mahali popote alipo na kufuatilia hatua zote za maombi yake kidijitali hadi anapopata huduma anayohitaji. Hii imepunguza gharama, muda na usumbufu kwa wananchi," amesema
Aidha, amebainisha kuwa jitihada za TBS katika kuboresha utendaji na utoaji wa huduma zimeendelea kutambuliwa kitaifa, baada ya Shirika hilo kushika nafasi ya tatu kati ya taasisi 47 za umma zilizoshindanishwa katika eneo la utawala bora kwenye utumishi wa umma mwaka huu, taasisi ya kwanza mwaka 2025 katika masuala ya udhibiti nchini na taasisi ya kwanza kwa mwaka 2023 Afrika.
Mwanasala amesema kuwa mafanikio hayo ni ishara ya dhamira ya TBS katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, huku akisisitiza kuwa Shirika hilo halitaridhika na mafanikio yaliyopatikana bali litaendelea kuboresha mifumo na huduma zake ili kukidhi mahitaji ya wananchi na wadau wa maendeleo.
Amewataka wananchi, wafanyabiashara na wazalishaji ambao hawajafika katika banda la TBS kutumia siku zilizobaki za maonesho hayo kutembelea banda hilo ili kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali zinazohusu ubora na usalama wa bidhaa.
"Tunawakaribisha wananchi wote kufika katika banda la TBS. Tunayo elimu, tunayo huduma na tunayo suluhisho la changamoto mbalimbali zinazohusu viwango. Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata bidhaa zenye ubora na salama," amesema

Social Plugin