Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADINI YA UJENZI UTAJIRI UNAO BADILI MAISHA YA WANANCHI WA HALI YA CHINI DODOMA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Madini ya ujenzi mchanga, kokoto na mawe yameendelea kuwa uti wa mgongo wa maisha ya kila siku Kwa watu wa chini bila kupata umaarufu unaolingana na mchango wake.

Madini haya huenda yasichukuliwe kama dhahabu wala kuzungumzwa kama tanzanite, lakini ndiyo yanayobeba msingi wa Tanzania ya leo.

Ni sekta inayojenga Tanzania kimyakimya, ikibeba uzito wa barabara, shule, hospitali na makazi ya wananchi, huku wakati huo huo ikiwa chanzo cha ajira na kipato kwa maelfu ya watu wa kipato cha chini.

Katika vumbi la machimbo ya Dodoma, ukweli mmoja unajitokeza wazi kwamba nyuma ya kila jengo linalovutia, kuna mikono ya vijana, wanawake na madereva wanaotegemea sekta hii kuendesha maisha yao.

Kwao, mchanga na kokoto si malighafi tu ni chakula, elimu na matumaini ya kesho.

Hata hivyo, pamoja na mchango wake mkubwa, sekta hii bado inakabiliwa na changamoto za kutotambulika kikamilifu katika sera kuu za uchumi wa madini.

Hili linahitaji mwelekeo mpya wa kimkakati ili kuhakikisha rasilimali hii inawanufaisha wananchi kwa uendelevu zaidi.

Kwa ujumla, madini ya ujenzi ni ushahidi kwamba maendeleo ya taifa hayajengwi na rasilimali za thamani kubwa pekee, bali pia na zile zinazoonekana kuwa za kawaida lakini zina mguso wa moja kwa moja kwa maisha ya watu wengi.

Kwa mujibu wa Tume ya Madini (2025), bei ya tani moja ya mchanga Dodoma ni wastani wa Shilingi 6,670, huku kokoto ikifikia zaidi ya Shilingi 34,000 na katika maeneo yenye uhitaji mkubwa, bei hupanda zaidi ya mara mbili.

Hamisi Mfaume ni mmoja wa wanufaika wa madini haya kutoka Kijiji Cha Mtumba Dodoma,anasema Kwa sasa maisha yake yamebadikika Kutoka vumbi la machimbo hadi umiliki wa lori
Katika machimbo ya Msanga Chamwino.

Anasema anakumbuka maisha yake ya zamani kwa tabasamu la ushindi.

“Nilikuwa naishi bila kuwa na uhakika wa kipato ,sikuwa na ajira napiga vibarua tu machimboni,Siku moja sina kazi, kesho sina uhakika lakini leo nina lori langu, na nimeajiri vijana wawili,” anasema.

Kwa Hamisi, madini ya ujenzi yamekuwa daraja kutoka maisha ya utegemezi kwenda ujasiriamali.

“Kila mzigo wa kokoto unaopita hapa ni chakula cha nyumbani kwangu,” anaongeza.

Kwa upande wake Marian James anasema Mawe yamebeba familia yake akiwa katika hali ya ujane.

Katika machimbo ya Nzuguni, mama mjane huyu mwenye watoto wanne, anaanza siku yake kabla ya jua kuchomoza.

Anakusanya mawe madogo, kuyaponda na kuyauza kwa mafundi ujenzi.

“Hapa nimeweza kujenga chumba changu, nimesomesha mtoto wangu mkubwa,bila machimbo haya nisingeweza kusimama,” anasema kwa sauti ya utulivu.

Kwa Mariam, kila jiwe si jiwe tu bali ni ada ya shule, ni chakula, ni maisha na ajira.

Kwenye simulizi hii ninushahidi wa kuwa katika pembe nyingi za Tanzania, mchanga unaochimbwa, kokoto zinazopondwa na mawe yanayovunjwa si tu malighafi za ujenzi ni msingi wa maisha ya maelfu ya wananchi wa kipato cha chini.

Hata hivyo, sekta hii imeendelea kubaki kivulini licha ya kuwa injini ya kila mradi wa maendeleo nchini.

Dondoo za msingi za uchunguzi
Kila barabara, daraja, shule na hospitali hutegemea madini ya ujenzi
Sekta hii inaajiri maelfu ya wananchi moja kwa moja na kwa njia zisizo rasmi
Wanufaika wakubwa ni vijana, wanawake wajane na madereva wa malori.

Hasheem Said ni muuzaji wa madini ujenzi Dodoma mjini anasema bei za mchanga na kokoto hutofautiana hadi mara 10 kulingana na mkoa .

Anasema madini ya ujenzi ni Sekta inayojenga taifa bila kutambuliwa
Katika maeneo ya Dodoma, Kongwa, Chamwino na Bahi, mashimo ya mchanga na machimbo ya kokoto yamegeuka kuwa “viwanda vya ajira” visivyo rasmi.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Dodoma (RMO) Medard Msengi anasisitiza kuwa sekta hii inakua kwa kasi lakini bado inahitaji usimamizi imara ili pande zote zinufaike.

“Changamoto kubwa ni uchimbaji usio rasmi na athari za mazingira, lakini mchango wake kwenye ajira ni mkubwa sana,” anasema.

“Hakuna barabara, reli, hospitali au shule inayojengwa bila madini haya,ni sekta inayogusa maisha ya kila Mtanzania moja kwa moja.”amesema

Anasema katika maeneo mengi ya vijijini, sekta hii imefungua mnyororo wa ajira ambapo Vijana wachimbaji na wanapondaji mawe kuwa kokoto.

"Kwa ujumla kila mtu ni mnufaika ,Madereva wa malori ya mchanga na kokoto,Wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi,Mama lishe wanaouza chakula machimboni,hii inaifanya sekta ya madini ya ujenzi kuwa moja ya sekta zenye mguso wa moja kwa moja kwa wananchi wa kipato cha chini,"amesema Msengi

Amesema Pamoja na mchango wake mkubwa, sekta hii inakabiliwa na Changamoto zinazotishia uendelevu wake ikiwemo Uharibifu wa mazingira na mashimo yasiyorejeshwa,Biashara isiyo rasmi ambayo inapunguza mapato ya Serikali na Ukosefu wa mitambo ya kisasa.

Naye Mjiolojia kutoka STAMICO Revocatus Mafungo anasema madini ya ujenzi ndiyo msingi wa miradi yote ya maendeleo nchini.
“Watu wengi huona madini ni dhahabu tu, lakini ukweli ni kwamba kila jengo kubwa linaanzia kwenye mchanga na kokoto,” anasema.

Kwa mtazamo wa uchunguzi huu, madini ya ujenzi si rasilimali za kawaida kama ambavyo wengi wamekuwa wakiamini.Ni mtaji unaowainua wananchi wa kipato cha chini kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye kujitegemea, huku ukiwezesha ujenzi wa miundombinu inayochochea maendeleo ya taifa.

Kila kokoto, jiwe na mchanga unaotolewa ardhini hubeba hadithi ya familia inayopata chakula, mtoto anayesoma na kijana anayepata ajira.

Hata hivyo, ili sekta hii iendelee kuwa chachu ya maendeleo, kuna haja ya kuimarisha usimamizi wa uchimbaji, kulinda mazingira, kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo na kuongeza uwekezaji katika teknolojia za kisasa.
Hatua hizo zitasaidia kuongeza mapato ya Serikali, kuboresha usalama wa wachimbaji na kuhakikisha manufaa ya rasilimali hizi yanawafikia wananchi wengi zaidi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Madini ya ujenzi yanaweza yasiangaze kama dhahabu au almasi, lakini thamani yake inaonekana kwenye nyumba zinazokamilika, barabara zinazounganisha jamii, shule na hospitali zinazohudumia wananchi, na zaidi katika maisha ya maelfu ya Watanzania wanaoyategemea kila siku.

Ndiyo maana, kwa hakika, madini ya ujenzi ni utajiri unaobadili maisha ya wananchi wa hali ya chini na nguzo muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea maendeleo jumuishi.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com