Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WAHIMIZWA KUTUNZA MAZINGIRA NA VYANZO VYA MAJI - KISHAPU

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambaye ndiye mgeni rasmi, Afisa Tawala Fadhili Mvanga akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani kiwilaya yakifanyika Kata ya Maganzo Juni 5, 2026

Na Sumai Salum - Kishapu

-Miche 500 yagawiwa kwa Wananchi ikiwemo ya vivuli,matunda na mbao

-Miche zaidi ya 350 imepandwa

Shirika la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS), kwa ufadhili wa kifedha kutoka Shirika la Norwegian Church Aid (NCA), limefanikisha kwa mafanikio makubwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo wadau mbalimbali wa mazingira walikutana kuhamasisha utunzaji wa mazingira, upandaji miti na usafi wa maeneo ya huduma za jamii.


Maadhimisho hayo yalienda sambamba na shughuli za upandaji miti katika Kituo cha Afya Masagala, usafi wa mazingira pamoja na utoaji wa vyeti vya pongezi kwa taasisi, mashirika na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa "Dira 2025: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania."

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mgeni Rasmi ambaye ni Afisa Tarafa wa Kishapu, Fadhili Mvanga, amepongeza TCRS na NCA kwa kuendelea kuwekeza katika shughuli za maendeleo ya jamii hususan uhifadhi wa mazingira.

Amesema wadau wa maendeleo wamekuwa nguzo muhimu katika kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kushirikiana na Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi endelevu.


"Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na TCRS pamoja na Norwegian Church Aid katika kuhamasisha jamii kutunza mazingira. Haya si maadhimisho ya siku moja pekee bali ni mwanzo wa dhamira ya kudumu ya kuhakikisha tunarithisha kizazi kijacho mazingira salama na yenye uhai. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kupanda miti, kuitunza na kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya Taifa letu," amesema Mvanga.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika kampeni za upandaji miti na usafi wa mazingira huku akisisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi hayawezi kupatikana bila kuwa na mazingira bora na salama.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Maganzo, Mhe. Hamza Tandiko, amesema viongozi wa kata hiyo wanaendelea kusimamia kwa karibu shughuli za utunzaji wa mazingira na upandaji miti ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa ya kijani na yenye kuvutia.

Amesema upatikanaji wa maji kutoka Ziwa Victoria umeongeza fursa ya wananchi kupanda na kutunza miti kwa urahisi zaidi.

"Tunatoa wito kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kutupatia miche ya kutosha ya miti. Pia wananchi watumie fursa zilizopo ikiwemo kupata miche katika maeneo mbalimbali kama Mwadui ili kuhakikisha kila kaya inapanda miti. Tunahitaji Maganzo na Kishapu kwa ujumla kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira nchini," amesema Tandiko.

Naye Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Cassim Said, amesema Halmashauri imeendelea kuweka sera, mikakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha mazingira yanatunzwa na sheria zote za mazingira zinatekelezwa ipasavyo.

Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhamasisha upandaji miti katika taasisi za umma, shule, vituo vya afya na makazi ya wananchi pamoja na kuimarisha elimu ya mazingira kwa jamii.


"Halmashauri itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu uhifadhi wa mazingira. Tunataka kuona kila mwananchi anakuwa mshiriki wa moja kwa moja katika kulinda mazingira kwa kupanda miti, kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji na kusimamia usafi katika maeneo yao," amesema Cassim Said.


Akizungumza kwa niaba ya TCRS Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Sanyenge, amesema shirika hilo linaamini kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila uwepo wa mazingira bora.


Amesema TCRS imeendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi kupitia uhifadhi wa mazingira, usimamizi wa rasilimali za asili na uhamasishaji wa jamii.


"Tunajivunia kuona wananchi wa Kishapu wanaitikia kwa vitendo wito wa kutunza mazingira. Kupitia ufadhili wa Norwegian Church Aid, tumeweza kufanikisha shughuli hizi ambazo zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustawi wa jamii. Tutaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," amesema Sanyenge.


Kwa upande wake, mwakilishi wa Norwegian Church Aid (NCA), Emmanuel Temu, amesema taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na mashirika ya maendeleo katika kulinda mazingira kwa kuwa ni msingi wa maisha na maendeleo ya wananchi.


"Mazingira ni urithi wetu wa pamoja. Norwegian Church Aid inaamini kuwa uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira ni uwekezaji katika afya, uchumi na ustawi wa jamii. Tunaendelea kushirikiana na TCRS kwa sababu tunaona matokeo chanya yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja," amesema Temu.

Naye mwananchi wa Kijiji cha Bulima, Kata ya Idukilo, Constantine Weja, amesema mafunzo na elimu wanayoendelea kuipata kuhusu mazingira imewasaidia kutambua umuhimu wa miti katika kuboresha hali ya hewa na maisha yao ya kila siku.


"Miti ni maisha yetu. Inatulinda dhidi ya ukame, inatunza vyanzo vya maji na kuboresha mazingira yetu. Tutaendelea kuwa mabalozi wazuri wa mazingira katika vijiji vyetu," amesema Weja.

Kwa upande wake, mwananchi wa Maganzo, Valentina Gayagamba, amesema ameshuhudia manufaa makubwa yatokanayo na utunzaji wa mazingira na upandaji miti ikiwemo kuboreka kwa hali ya hewa na kuongezeka kwa kivuli katika maeneo mbalimbali ya makazi.


"Elimu tunayoipata inatupa uelewa mkubwa wa namna mazingira yanavyohusiana na maisha yetu. Tumejifunza kuwa kila mti tunaoupanda leo ni uwekezaji wa kesho kwa watoto wetu na jamii kwa ujumla," amesema Valentina.



Maadhimisho hayo yameacha ujumbe mzito kwa wananchi wa Kishapu kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja, huku ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii ukiendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya kujenga Tanzania ya kijani na endelevu.
Diwani wa Kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhe.Hamza Tandiko akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani Wilayani Kishapu yaliyofanyika Kata ya Maganzo Juni 5,2026
Afisa Tarafa ya Mondo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Atka Haji akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani Wilayani Kishapu yaliyofanyika Kata ya Maganzo Juni 5,2026
Afisa mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Cassim Said akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani Wilayani Kishapu yaliyofanyika Kata ya Maganzo Juni 5,2026
Mwakilishi kutoka Shirika la Tanganyika Christian Refuge Service (TCRS) mkoani Shinyanga Emmanuel Sanyenge akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani Wilayani Kishapu yaliyofanyika Kata ya Maganzo Juni 5,2026
Mwakilishi kutoka Shirika la Norwegian Church Aid Emmanuel Temu akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani Wilayani Kishapu yaliyofanyika Kata ya Maganzo Juni 5,2026

Mwenyekiti wa Kijiji Cha Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Shishi Jagadi
Mhifadhi wa Wakala wa Misitu na uhifadhi TFS wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Tumaini Masatu
Mtendaji wa Kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Stephen Yalomba




















































































































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com