Na Mwandishi Wetu
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amesema kuwa kukosoa ni haki ya msingi katika jamii ya kidemokrasia, lakini ukosoaji huo unapaswa kufanywa kwa kuzingatia maadili, heshima na ukweli.
Akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Barnabas Lucas, baada ya kuwasilisha mada kuhusu “Uhuru wa Vyombo vya Habari katika Enzi ya Kidijiti: Wajibu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari” katika Kongamano la Uhuru wa Vyombo vya Habari lililoandaliwa na UDOM kupitia Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari.
Wakili Kipangula amezungumza mipaka ya uhuru wa kujieleza na ukosoaji wa viongozi katika jamii. Amesisitiza kuwa wananchi wana haki ya kutoa maoni na kukosoa, lakini wanapaswa kufanya hivyo kwa lugha yenye staha na inayojenga.
“Kukosoa siyo kosa, lakini kukosoa siyo kutukana. Kukosoa siyo kubagua, na kukosoa siyo kudhalilisha. Tunapaswa kutofautisha kati ya kutoa hoja za kujenga na kutumia lugha inayovunja maadili na kuhatarisha mshikamano wa jamii,” alisema Kipangula.
Ameongeza kuwa uhuru wa kujieleza unaambatana na wajibu wa kuhakikisha kuwa taarifa na maoni yanayotolewa yanazingatia sheria, maadili na maslahi ya umma.
“Jamii inahitaji watu wanaotoa mawazo na mitazamo tofauti kwa lengo la kuleta maendeleo. Hata hivyo, tofauti za mawazo zisigeuke kuwa chanzo cha matusi, chuki au uvunjifu wa heshima kwa wengine,” amesisitiza .
Kipangula amesema elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na mawasiliano ya umma ni muhimu katika kuwajengea wananchi, hususan vijana, uwezo wa kushiriki mijadala ya kitaifa kwa njia yenye staha, uwajibikaji na tija.

Social Plugin