
Upotoshaji na usambazaji wa taarifa za uongo mitandaoni umekuwa tishio kubwa linalovuruga na kuyumbisha amani, huku ukisababisha athari mbaya kama utapeli, matusi na uzushi katika jamii.
Aidha, upotoshaji huo unasababisha upotevu mkubwa wa fedha kupitia taarifa za kitapeli na hata kushuka kwa afya ya akili kunakochangiwa na unyanyasaji au msongo wa mawazo mtandaoni.
Si siri kuwa taarifa hizo hutumika kupotosha umma kuhusu taasisi au mamlaka fulani ili kulaghai wananchi, hali inayosababisha hasara na kupoteza uaminifu wa kibiashara sambamba na kuenea kwa migogoro.
Kwa muktadha wa Tanzania, upotoshaji wa makusudi huwafikisha wahusika katika mikono ya sheria kupitia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015. Izingatiwe kuwa, watu wanapopewa taarifa zisizo sahihi hufanya uamuzi usio sahihi unaosababisha madhara na majuto makubwa kwao na kwa jamii zao.
Kwa mfano, wakati wa matukio muhimu ya kitaifa au kijamii, uzushi unaweza kuibua hofu, taharuki au mkanganyiko miongoni mwa wananchi, hali inayokwamisha maendeleo ya watu. Kutokana na athari hizo, Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, David Misime, na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamekuwa wakisisitiza wananchi kutosambaza taarifa za uzushi, upotoshaji, matusi na uchochezi, na badala yake kuripoti udanganyifu au uhalifu huo katika vyombo husika.
Endapo watumiaji wa mitandao ya kijamii watakuwa makini na kuwajibika, jamii itanufaika na teknolojia ya mawasiliano bila kuathiriwa na upotoshaji wa taarifa kwani utaepukwa.
Social Plugin