Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GRAND CHALLENGES TANZANIA YATAJWA KUWA CHACHU YA UCHUMI WA MAARIFA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Serikali imesema maendeleo ya uchumi wa Tanzania yanahitaji kuungwa mkono na uwekezaji mkubwa katika tafiti, ubunifu na teknolojia ili kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za ndani katika soko la kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa programu ya Grand Challenges Tanzania, jukwaa jipya linalolenga kuhamasisha watafiti, wabunifu na taasisi mbalimbali kuibua suluhisho za changamoto za maendeleo kupitia sayansi na teknolojia.

Akizindua programu hiyo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, alisema mpango huo utasaidia kuunganisha maarifa ya wataalamu wa ndani na mahitaji halisi ya wananchi ili kuzalisha bunifu zenye matokeo ya moja kwa moja katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Alisema Serikali inaamini matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususan katika kukabiliana na changamoto za afya, usalama wa chakula na mazingira.

Mwenyekiti wa Bodi ya Grand Challenges Tanzania, Ladislaus Mnyone, alisema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunategemea uwezo wa nchi kuwekeza katika maarifa, tafiti na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini

Alieleza kuwa ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia utaongezeka zaidi iwapo kutakuwa na mazingira yanayowezesha wabunifu na watafiti kuendeleza teknolojia zinazojibu mahitaji ya wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Amos Nungu, alisema programu hiyo itakuwa daraja la kuwakutanisha watafiti, sekta binafsi na taasisi za umma ili kubuni majawabu ya changamoto zinazoikabili jamii.

Naye Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Islam Seif Salim, alisema mpango huo una nafasi kubwa ya kuibua teknolojia mpya, kuvutia uwekezaji na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta muhimu za maendeleo.

Programu ya Grand Challenges Tanzania inalenga kujenga mfumo unaounganisha sayansi, teknolojia na ubunifu wa ndani kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya taifa na kukuza uchumi unaotegemea maarifa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com