Na Dotto Kwilasa,Dodoma
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi bilioni 334.3 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na vipaumbele mbalimbali vya sekta hiyo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha Mpango wa Mapato na Matumizi wa Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii Ashatu Kijaji alisema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 272 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 62.3 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Dkt. Kijaji alisema fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali zikiwemo usimamizi wa sekta, utoaji wa huduma, utekelezaji wa sera pamoja na kuendeleza vivutio vya utalii na kuboresha huduma za ukarimu nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema sekta ya utalii imeendelea kufanya vizuri ambapo idadi ya watalii nchini imeongezeka hadi kufikia watalii 5,935,561 mwaka 2025 kutoka watalii 5,360,247 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 10.7.
Alisema watalii wa kimataifa waliongezeka kwa asilimia 13.1 kutoka watalii 3,218,352 mwaka 2024 hadi kufikia watalii 3,641,066 mwaka 2025, huku watalii wa ndani wakiongezeka kwa asilimia 7.1 kutoka watalii 2,141,895 mwaka 2024 hadi watalii 2,294,495 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha hifadhi za taifa pamoja na kampeni za kimataifa za kuitangaza Tanzania kama kivutio kikuu cha utalii duniani.
Aidha, alisema taarifa ya Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 11 duniani kwa ongezeko la wageni wa kimataifa kwa asilimia 51 ikilinganishwa na mwaka 2019 kabla ya janga la UVIKO-19.
Aliongeza kuwa Tanzania pia imekuwa ya sita Afrika na kushika nafasi ya tatu duniani kwa upande wa matumizi ya watalii, hali inayodhihirisha kuimarika kwa mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara kupitia Idara ya Utalii itaendelea kusimamia maendeleo na udhibiti wa sekta hiyo kwa lengo la kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa pamoja na kuboresha huduma kwa watalii.
Alisema Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya maendeleo ya utalii endelevu ikiwemo kuendeleza vivutio vya utalii katika Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini, Pwani na Kanda ya Ziwa ili kuongeza idadi ya watalii pamoja na mapato ya sekta hiyo.
Pia Wizara itaandaa Mpango Kabambe wa Uendelezaji Utalii Nchini utakaoweka mwelekeo wa kukuza sekta hiyo kwa kushirikisha sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuvutia uwekezaji mkubwa katika biashara za utalii nchini.
Sambamba na hilo, Wizara itaendelea kuibua vivutio vipya vya utalii, kuboresha ubora wa huduma za utalii na ukarimu pamoja na kuandaa mikakati ya motisha za uwekezaji ili kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wawekezaji.
Katika kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo, Wizara itafanya mapitio ya Sheria ya Utalii Sura ya 65 pamoja na kanuni zake kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa biashara za utalii na ukarimu nchini.
Aidha, itaendelea kufanya ukaguzi wa biashara za utalii, kupanga huduma za malazi na chakula pamoja na kuweka viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa kwa watalii.
Kwa upande wa maendeleo ya wataalamu wa sekta hiyo, Wizara itaratibu usajili wa wataalamu wa utalii na ukarimu pamoja na kuandaa kanzidata maalumu kwa ajili ya kupanga maendeleo ya kada mbalimbali katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji alisema Wizara hiyo imejipanga kutekeleza vipaumbele tisa katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Alivitaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni kuimarisha utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi, kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa meli, mikutano na matukio (MICE), fukwe, michezo, anga na tiba pamoja na kuboresha miundombinu katika maeneo ya utalii na hifadhi.
Pia Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale kwa kushirikisha jamii pamoja na kupambana na ujangili na uharibifu wa mazingira.
Vilevile, Wizara imepanga kuongeza matumizi ya teknolojia kisasa katika usimamizi wa rasilimali, ukusanyaji wa mapato, ufuatiliaji pamoja na shughuli za utangazaji wa utalii.
Dkt. Kijaji alisema Serikali pia itaendelea kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia sambamba na kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji katika sekta ya maliasili na utalii



Social Plugin