Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limeendelea na kikao chake cha bajeti ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii imewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27, yakilenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kuongeza mapato ya utalii na kuendeleza rasilimali za taifa kwa manufaa ya wananchi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo Bungeni leo Mei 15, 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 wizara imejipanga kutekeleza vipaumbele tisa vikuu vinavyolenga kuimarisha uhifadhi wa rasilimali, kukuza utalii na kuongeza tija ya sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Amesema vipaumbele hivyo vitazingatia mageuzi ya kimkakati katika usimamizi wa maliasili na kukuza sekta ya utalii nchini na kwamba kipaumbele cha kwanza ni kuimarisha uhifadhi, ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale ili kuhakikisha rasilimali hizo zinachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa bila kuharibiwa.
Ametaja kipaumbele cha pili ni kuboresha miundombinu wezeshi katika maeneo ya utalii na hifadhi, ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano na huduma za kijamii ili kurahisisha upatikanaji wa vivutio vya utalii.
"Tutaimarisha utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi kwa kutumia mikakati mahsusi ya masoko, ikiwemo kuelekeza nguvu katika masoko ya Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati, pamoja na kutumia fursa za kimataifa kama AFCON 2027, IPU, mashindano ya ulimbwende wa dunia na tuzo za ubora za utalii zinazoandaliwa na WTA zitakazofanyika nchini,"amesema
Ameeleza kuwa wizara hiyo pia itaendeleza na kuboresha mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa meli, mikutano na matukio (MICE), pamoja na kutambua na kusajili mazao mapya ya utalii ili kuongeza ushindani wa sekta hiyo kimataifa.
Vipaumbele kingine ni kuimarisha uzalishaji, uongezaji thamani na masoko ya mazao ya misitu na nyuki ili kuongeza kipato kwa wananchi wanaojihusisha na sekta hiyo na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa rasilimali, ulinzi, ufuatiliaji, ukusanyaji wa mapato pamoja na utangazaji wa utalii ili kuongeza ufanisi na uwazi.
"Pamoja na vipaumbele hivyo pia tutaimarisha utafiti, ubunifu na maendeleo ya rasilimaliwatu katika sekta ya maliasili na utalii ili kuongeza weledi na ufanisi wa watendaji na kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia,"ameeleza



Social Plugin