Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SWICA YAIBUA MATOKEO CHANYA KISESA


Na Beatus Maganja , Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Musa Godfrey Mbunga, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuanzisha utaratibu wa Uwekezaji Mahiri wa maeneo ya uhifadhi ujulikanao kama Special Wildlife Investment Concession Areas (SWICA), akisema mfumo huo umeleta manufaa makubwa kwa wananchi wanaoishi jirani na Hifadhi ya Maswa mkoani Simiyu.

Mhe. Mbunga alitoa pongezi hizo bungeni jijini Dodoma tarehe 15 Mei, 2026 wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema utekelezaji wa utaratibu huo umewezesha wananchi wa maeneo mbalimbali ndani ya jimbo lake kunufaika moja kwa moja na mapato yatokanayo na uwekezaji unaofanyika katika maeneo ya uhifadhi.

“Wizara imeanzisha utaratibu wa Uwekezaji Mahiri (SWICA), na utaratibu huu umesaidia sana wananchi kunufaika na uwekezaji unaofanyika kwenye Hifadhi ya Maswa,” alisema Mhe. Mbunga.

Mbunge huyo alieleza kuwa kupitia mfumo huo, jimbo la Kisesa limepokea takribani shilingi milioni 973 zilizosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo tofauti ya jimbo hilo.

Alifafanua kuwa kijiji cha Matale kilipokea zaidi ya shilingi milioni 390 zilizotumika kujenga zahanati, nyumba za watumishi pamoja na wodi ya wazazi.

Aidha, alisema maeneo ya Ng’hanga na Bulyandulu kila moja lilipata shilingi milioni 181 zilizosaidia ujenzi wa nyumba za watumishi, huku Mbugayabang’hya ikinufaika na shilingi milioni 216 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Mhe. Mbunga amesema mafanikio hayo yanaonesha namna Serikali inavyoendelea kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo ya uhifadhi wananufaika na rasilimali za taifa kupitia uwekezaji wenye tija.

“Ni lazima kuishukuru Serikali kwa hatua hizi ambazo zimeendelea kuleta maendeleo kwa wananchi wetu,” alisisitiza.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Mhe. Waziri Dkt . Ashatu kijaji (Mb) imeendelea kusisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za uhifadhi na uwekezaji ili kuhakikisha rasilimali za maliasili zinachangia maendeleo ya jamii pamoja na uchumi wa Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com