Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amesema kukosekana kwa usikivu, utiifu na kuheshimu mamlaka ni miongoni mwa sababu zinazochochea kuvunjika kwa amani na kuibuka kwa migogoro katika jamii.
Akizungumza wakati wa ibada ya Eid Al-Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma leo Mei 27 ,Sheikh Mustapha amesema jamii inapopuuza mamlaka zilizowekwa na kushindwa kusikilizana, hali hiyo husababisha migawanyiko, vurugu na hata umwagaji damu.
Amesema amani ya taifa hujengwa kupitia misingi ya kuheshimiana, kusikilizana na kuzingatia sheria pamoja na maelekezo ya viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza jamii.
“Moja ya chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani ni watu kukosa utiifu kwa mamlaka na viongozi waliopo madarakani, jambo ambalo mara nyingi husababisha vurugu na machafuko katika jamii,” amesema.
Aidha, amewasisitiza wananchi kuendelea kuheshimu taasisi mbalimbali za kijamii na kidini pamoja na vyombo vinavyoundwa kusimamia masuala ya wananchi, ikiwemo tume na kamati za kidini.
Kwa mujibu wake, taifa lenye wananchi wanaoheshimu maamuzi ya viongozi na taasisi halali huwa na utulivu, mshikamano pamoja na mazingira mazuri ya maendeleo.
Akizungumzia maadhimisho ya Eid Al-Adha, Sheikh Mustapha amesema siku hiyo ni ya kihistoria kwa Waislamu na inabeba mafunzo makubwa ya utiifu, uvumilivu na kumtii Mwenyezi Mungu.
Ameeleza kuwa simulizi ya Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail inaonyesha namna ambavyo waumini wanapaswa kuwa na usikivu, utiifu na kuheshimu maagizo ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya kila siku.
“Hadithi ya Nabii Ibrahim na Nabii Ismail si simulizi ya kawaida, bali ni funzo linalotukumbusha umuhimu wa kusikilizana, kuheshimiana na kutii mamlaka,” amesema.
Pia amewahimiza Waislamu wenye uwezo kutekeleza ibada ya kuchinja wakati wa Eid Al-Adha kama ilivyoelekezwa katika mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Katika hitimisho lake, Sheikh huyo alisisitiza kuwa dini inawaelekeza waumini kumtii Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad pamoja na viongozi wa serikali, dini na jamii kwa ujumla ili kuendelea kudumisha amani na mshikamano wa taifa.


Social Plugin