Na Bora Mustafa, Arusha.
Wakili Mkuu wa Serikali, Ally Possi amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikiwa kushinda mashauri 565 kati ya mashauri 641 yaliyoidhinishwa na ofisi hiyo, sawa na asilimia 88.1 ya mashauri yote yaliyomalizika, pamoja na kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 316.28 katika mwaka wa fedha uliomalizika Julai.
Amesema hayo leo mei ,18,2026 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa mawakili wa serikali, ambapo ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kujenga serikali yenye uwezo wa kusimamia mashauri kwa weledi pamoja na kuandaa kizazi cha mawakili wa serikali wenye uwezo wa kulitumikia taifa kwa ufanisi.
Aidha, Dkt. Possi amesema mabadiliko yanayoendelea katika sekta mbalimbali nchini yanahitaji pia mabadiliko ndani ya sekta ya sheria, hasa katika matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria.
Amesema mawakili wa serikali wanapaswa kuendelea kujitolea kwa ari kubwa katika kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi pamoja na kusaidia kuzuia migogoro inayoweza kuathiri maendeleo ya taifa.
Pamoja na hayo, amesema mashauri yote ikiwemo ya madai na usuluhishi (arbitration) yaliyoendeshwa kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026 yameiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuokoa takribani shilingi trilioni 1.35.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Zuberi Homera amesema serikali inaamini kuwa hakuna maendeleo endelevu wala uchumi shindani bila kuwepo kwa utawala bora wa sheria.
Amesema taifa linahitaji viongozi pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia haki kwa uadilifu huku akisisitiza kuwa usimamizi mzuri wa mashauri ya serikali pamoja na nidhamu katika utendaji vitasaidia taifa kufikia dira ya maendeleo ya mwaka 2030.
Aidha, amesema Watanzania wana imani kubwa kwa wataalamu wa sheria, hivyo wanapaswa kuwa mfano wa maadili mema, uzalendo pamoja na utoaji wa huduma bila upendeleo kwa wananchi.
Hata hivyo, Waziri Homera amesema serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaotoa maneno ya uchochezi pamoja na maadili yasiyofaa kwenye mitandao ya kijamii kwa kushirikiana na wizara husika ili kulinda maslahi ya taifa.
Pia amesema serikali inaendelea kushirikiana na mabaraza ya ardhi katika kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi inapatiwa ufumbuzi kupitia
vyombo vya sheria pamoja na mahakama.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Damasi Ndumbaro amesema Bunge ni mdau muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya sekta ya sheria pamoja na mahakama.
Amesema katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Bunge wamebaini kuwa baadhi ya sheria zimetungwa bila kufanyika tafiti za kutosha, hivyo ametoa wito kwa sekta husika kuhakikisha tafiti zinafanyika kabla ya kutungwa kwa sheria mpya.
Aidha, amesisitiza kuwa mashauri yanayoendeshwa yawe darasa la kusaidia kurekebisha mapungufu ya sheria zilizopo ili kujenga mfumo bora wa haki nchini.
Hata hivyo, amesema taifa linaendelea kukumbwa na migogoro mingi ya ardhi ambayo inaweza kusababisha athari kwa amani pamoja na uchumi wa taifa endapo haitadhibitiwa mapema.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Zanzibar, Shabani Abdla amesema taasisi mbalimbali zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha sekta ya sheria nchini.
Amesema mawakili wanapaswa kutumia mafunzo hayo kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi kwa haki pamoja na kulinda maslahi ya taifa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Elisante Ole Gabriel amesema ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo ni muhimu katika kuimarisha utoaji wa haki pamoja na kusaidia kizazi kijacho cha wataalamu wa sheria.
Kauli mbiu ya mafunzo hayo ni “Litigate, Arbitrate, Serve – Serving the State, Shaping the Future”, ambapo wadau takribani 600 kutoka sekta mbalimbali za sheria nchini wameshiriki.


Social Plugin