Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA KAZI KWA WATUMISHI WA UMMA



Na. Antonia Mbwambo-Arusha

Watumishi wa Umma nchini wamehakikishiwa kuboreshewa mazingira ya kazi kadri uchumi utakavyoruhusu ili kuleta tija katika utendaji kazi kwa maslahi ya umma.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika leo tarehe 12 Mei, 2026 katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha.

Mhe. Qwaray amesema, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Watumishi wa Umma wote nchini wakiwemo Wauguzi, hivyo itazingatia changamoto wanazokutana nazo watumishi hao, pamoja na kushughulikia kwa uzito unaostahili ili kutengeneza mazingira mazuri ya utendaji kazi.

"Niwahakikishie Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya Watumishi wa Umma kadri uchumi utakavyoruhusu kwani tunatambua mchango wenu mkubwa katika kuwahudumia Watanzania, fanyeni kazi, Serikali ipo nanyi." Mhe. Qwaray alisema.

Aidha Mhe. Qwaray ameongeza kuwa, ili kuwa na ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi Serikali itaendelea kuisimamia sekta ya afya pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma bila kuathiri misingi ya Utumishi wa Umma, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ikiwemo uzingatiaji wa maadili.

Aidha amewataka kuwa na kauli nzuri, huruma na upendo utakaoongeza tija katika utendaji kazi ili kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya afya.

Ninyi ndiyo watu wa kwanza kukutana na mgonjwa pindi anapofika hospitali na ni watu wa mwisho mgonjwa anapotoka hospitali baada ya matibabu, ikiwa mtakuwa na nyuso za ukatili na ulimi mkali au wa kebehi, mtawakwaza wagonjwa na hata kuwakatisha tamaa jambo ambalo litaonyesha mapungufu katika sekta ya afya.”Mhe. Qwaray alisema.

Vilevile, Mhe. Qwaray amewaahidi Wauguzi hao kuwa Ofisi imepokea masuala yote waliyoyaeleza katika risala yao na kuwaahidi kuyawasilisha kwa ajili ya kufanyiwa kazi ikiwemo masuala ya Muundo Mpya wa Utumishi wa Kada ya Uuguzi na Ukunga na Muundo wa Utawala katika Sekta ya Afya ili kuboresha huduma ya afya na maslahi ya watumishi wa afya nchini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Qwaray, ametoa wito kwa wauguzi kuhahakisha wanabadili mienendo na tabia zisizopendeza wala kuendana na maadili ya kazi yao, lakini pia amewapongeza kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kuwahudumia wananchi na kuboresha afya zao.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wauguzi (TANNA), Dkt. Ezekiel Mbao amemshukuru Naibu Waziri, Mhe. Regina Qwaray kwa kujumuika nao kwenye maadhimisho ya siku hiyo adhimu.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Wauguzi Duniani yamebeba kauli mbiu isemayo Wauguzi Wetu, Mustakabali Wetu, Wauguzi Waliowezeshwa Huokoa Maisha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com