Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

OPERESHENI YA JESHI LA POLISI SHINYANGA YANASA WAHAMIAJI HARAMU 11

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata wahamiaji haramu 11 waliokuwa wameingia na kuishi nchini bila vibali halali katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth magomi ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyotokea katika kipindi cha mwezi mmoja ikiwa ni pamoja na kukamata watuhumiwa 78.

Amesema kupitia operesheni hizo, polisi wamekamata vielelezo mbalimbali,ambavyo ni lita za mafuta ya dizeli 480, mabati 558, kete 228 za bangi, lita 115 za pombe haramu aina ya moshi, kilogramu 89 za mirungi, pikipiki 11 pamoja na betri tatu za magari.

Katika hatua nyingine ,Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kurejesha silaha moja aina ya bastola TISAS yenye namba za usajili T0620-22J00122 pamoja na risasi 11 zilizokuwa ndani ya magazine, silaha ambayo iliripotiwa kuibwa Mei 10, 2026 katika mtaa wa Nyakato, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kamanda Magomi amesema bastola hiyo ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Richard Mhabi (38), mfanyabiashara na mkazi wa Nyakato Kahama.

Amesema baada ya jeshi hilo kufanya uchunguzi wa kina pamoja na operesheni maalumu, watuhumiwa wawili walikamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwa sasa wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kutoa rai kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kusaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com