Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAZINDUA MFUKO WA KUCHANGIA MATIBABU YA FIGO,UROTO





Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imezindua rasmi mfuko maalum wa kuchangia matibabu ya figo na uroto wenye lengo la kukusanya Sh bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili ili kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji kupata huduma za kibingwa ambazo zimekuwa na gharama kubwa kwa wananchi wengi.

Mfuko huo umeanzishwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo tangu ianze kutoa huduma zake, hatua inayolenga kuimarisha zaidi huduma za kibobezi nchini hususan upandikizaji figo na uroto.

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk. Henry Humba,amezungumza hayo Leo Mei 21,2026 Jijini Dodoma na kueleza kiwa mfuko huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma muhimu za afya na kuhakikisha wananchi wanapata tiba ndani ya nchi bila kulazimika kwenda nje.

Amesema huduma za upandikizaji figo na uroto ni za gharama kubwa, hivyo uanzishwaji wa mfuko huo utasaidia kupunguza changamoto ya wagonjwa wasio na uwezo wa kifedha kupata matibabu hayo muhimu.

“Maadhimisho haya ya miaka 10 yanalenga kuimarisha huduma za kibingwa nchini. Kupitia mfuko huu tunataka kuhakikisha hakuna mgonjwa anayekosa huduma kwa sababu ya gharama,” amesema Dk. Humba.

Amebainisha kuwa hospitali hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na maendeleo ili kuhakikisha mfuko huo unafanikiwa, huku akieleza kuwa tayari mafanikio yameanza kuonekana ambapo zaidi ya wagonjwa 55 wamefanyiwa upandikizaji figo na watoto 28 wamepata huduma ya upandikizaji uroto.

Amesema mchango wa awali wa Sh bilioni 1 uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan umeonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha huduma hizo za kibingwa nchini.

Aidha, hospitali hiyo imeeleza kuwa uwekezaji unaoendelea unaifanya Tanzania kuendelea kujijengea sifa ya kuwa kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewahamasisha Watanzania na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kuchangia mfuko huo ili kusaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma hizo muhimu.

Amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia BMH yameonesha uwezo mkubwa wa nchi katika kutoa huduma za kibingwa ndani ya Tanzania, huku akisisitiza kuwa mchango wa kila Mtanzania unaweza kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji matibabu hayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com