
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wambura Wagana akitoa salamu za benki ya CRDB
Meneja biashara wa CRDB Kanda Magharibi Anselm Mwenda akielezea huduma za CRDB kwa wafugaji mbele ya mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agness Meena alipotembelea banda la CRDB katika viwanja vya Busanda.
****
Benki ya CRDB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuimarisha sekta ya mifugo nchini kwa kuwa mdhamini mkuu wa Maonyesho ya Mifugo Kanda ya Ziwa yanayofanyika katika Viwanja vya Busanda mkoani Shinyanga.
Maonyesho hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya FarmFlex yanafanyika kwa siku mbili, kuanzia Mei 30 hadi 31, 2026, yakibeba kaulimbiu ya “Ufugaji Kibiashara”, yenye lengo la kuwajengea wafugaji uwezo wa kuongeza tija, thamani na faida katika shughuli zao za ufugaji.
Akizungumza katika maonyesho hayo, mbele ya mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agness Meena, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wambura Wagana, aliyeongoza ujumbe wa benki hiyo, amesema CRDB imejipanga kuwa mshirika wa karibu wa wafugaji nchini kupitia huduma mbalimbali za kifedha zinazolenga kukuza uchumi wao.
Ameeleza kuwa Benki ya CRDB imesaini makubaliano ya ushirikiano na Chama cha Wafugaji Tanzania kwa lengo la kuwawezesha wafugaji kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, sambamba na fursa za uwekezaji na maendeleo ya biashara zao.
“Kupitia kampuni yetu tanzu ya CRDB Foundation, tunatoa huduma za akaunti na mikopo ya IMBEJU kwa wafugaji binafsi pamoja na vikundi, ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kukuza shughuli zao za ufugaji kwa tija zaidi,” amesema Wagana.
Aidha, amesema kupitia kampuni tanzu ya CRDB Insurance Company, benki hiyo imeanzisha huduma ya Bima ya Mifugo, ambayo itawasaidia wafugaji kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali yanayoweza kusababisha upotevu wa mifugo na hasara za kifedha.
“Tunawahimiza wafugaji wote kutumia huduma ya bima ya mifugo ili kulinda uwekezaji wao dhidi ya hatari mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wowote,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Wagana amewajulisha wananchi na wafugaji kuwa Benki ya CRDB Busanda katika kipindi hiki cha maonesho ya mifugo huduma zote za kibenki zinapatikana kwa urahisi zaidi ikiwemo kufungua Akaunti, kuweka fedha, kutoa fedha na kuomba mikopo.
Amewataka wananchi na wafugaji kutumia fursa hiyo kupata huduma za akaunti, mikopo, bima na huduma nyingine za kifedha zinazotolewa na benki hiyo.
Ushiriki wa Benki ya CRDB katika maonyesho hayo unaakisi dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kusaidia maendeleo ya sekta ya mifugo na kilimo, ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania.











Social Plugin