
Na Hadija Bagasha Tanga
Wimbi la uvumi wa kupotea kwa sehemu za siri kwa wanaume, ambalo tayari limezua taharuki na matukio ya mashambulizi katika baadhi ya mikoa nchini, sasa limetua rasmi Mkoani Tanga, huku Jeshi la Polisi likianza kukabiliana nalo kwa hatua kali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Aprili 7, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, alisema watu watano wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika katika matukio mawili tofauti ya mashambulizi yaliyochochewa na uvumi huo.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchunguzi, “Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kumshambulia, kujeruhi na kuzua taharuki katika jamii,” akieleza kuwa matukio hayo ni matokeo ya imani potofu zinazoendelea kusambaa kwa kasi.
Katika tukio la kwanza lililotokea Aprili 5, 2026 majira ya saa 2 usiku katika Bar ya Kivuga Point, iliyopo Kijiji cha Mazingara wilayani Handeni, mkazi mmoja Santiel John alijikuta akipigwa kikatili baada ya kutuhumiwa kuhusika na madai ya kupotea kwa uume wa mmoja wa watuhumiwa.
Washukiwa wawili, Vado Mchungu na Fadhili Nuru, wanadaiwa kumshambulia kwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake wakiamini bila ushahidi kuwa ndiye chanzo cha tatizo hilo.
Hata hivyo, uchunguzi wa haraka wa Jeshi la Polisi ulibaini kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli. Kamanda Mchunguzi alisisitiza, “baada ya uchunguzi, mhusika aliyedai kupoteza uume wake alikutwa akiwa mzima na salama, hivyo tuhuma hizo hazikuwa na msingi wowote.”
Mhanga wa tukio hilo alikimbizwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu, huku watuhumiwa wote wawili wakiendelea kushikiliwa kituoni kwa mahojiano zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.
Katika tukio la pili lililotokea Aprili 6, 2026 majira ya saa 12:30 jioni katika eneo la Mabanda ya Papa, jijini Tanga, hali ya taharuki ilizuka ndani ya gari la abiria aina ya Hiace baada ya watu watatu kumtuhumu abiria mwenzao kuwa amewaondolea nyeti zao.
Watuhumiwa hao, Haji Mbwana, Mbwana Mluku na Amiri Rashid, walikamatwa mara moja na kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa uchunguzi wa kitabibu ili kubaini ukweli wa madai yao.
Kamanda Mchunguzi alibainisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa mara baada ya uchunguzi kukamilika, akionya kuwa “hakuna mtu anayepaswa kushambuliwa kwa misingi ya uvumi au hofu zisizo na uthibitisho.”
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo na kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu wasio na hatia.
Social Plugin