Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAHABARI WALIA NA VIZINGITI, SERIKALI YAKUMBUSHWA KULINDA UHURU


Wadau wa habari nchini wameeleza wasiwasi wao kuhusu mwenendo unaoendelea wa kudorora kwa uhuru wa vyombo vya habari, wakisisitiza kuwa hali hiyo inaweka hatarini misingi ya demokrasia.

Akizungumza  Leo Aprili 28,2025 jijini Arusha, Mwenyekiti wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), Ernest Sungura amesema kuwa tathmini ya hivi karibuni inaonesha hali ya uhuru wa vyombo vya habari bado hairidhishi, huku ikiendelea kuzalisha hofu miongoni mwa wanahabari nchini.

Aidha amesema tathmini hiyo imewasilishwa katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayoadhimishwa Mei 3, ambapo wadau wa habari wamekuwa wakifanya uchambuzi wa kina kuhusu hali halisi ya tasnia hiyo nchini Tanzania.

Pia amesema katika kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, amesema jumla ya matukio nane ya ukiukwaji dhidi ya wanahabari yameripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mbeya na Mwanza.

Amesema miongoni mwa matukio hayo, wanahabari wamekamatwa na kushikiliwa na polisi, wengine wakanyang’anywa vifaa vyao vya kazi, huku tukio moja likihusisha mwanahabari kuitwa kujieleza kuhusu maudhui ya mahojiano aliyofanya.

Amesema chombo kimoja cha habari kilifungiwa kwa siku 90, huku baadhi ya wanahabari waliokamatwa wakiachiliwa kwa dhamana baada ya kupatiwa msaada wa kisheria.

Kwa mujibu wa takwimu, amesema zaidi ya matukio 55 ya ukiukwaji dhidi ya wanahabari na vyombo vya habari yameripotiwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi mwaka 2025.

Hata hivyo ameongeza kuwa hali hiyo inaonesha hakuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na mwaka uliopita, ambapo matukio ya aina hiyo yaliendelea kuripotiwa katika kipindi kama hiki cha Januari hadi Aprili.

Amesema kuna haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti kulinda uhuru wa vyombo vya habari ili kuimarisha demokrasia na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com