Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TTCL YAKABIDHI MAGARI 9, BAJAJI 28 KUIMARISHA HUDUMA


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekabidhi rasmi magari tisa na bajaji 28 kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, likilenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya shirika hilo.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam, Aprili 29, 2026, yakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Moremi Marwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Marwa amesema jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimetumika kununua magari aina ya Toyota Hilux, huku shilingi milioni 291.2 zikitumika kununua bajaji hizo 28.
Moremi Marwa.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo umetokana na faida ya mwaka wa fedha 2024/25, ambapo shirika lilipata jumla ya shilingi bilioni 22.98.

“Lengo la uwekezaji huu ni kuimarisha huduma pamoja na miundombinu ya mawasiliano nchini,” amesema Marwa.

Ameongeza kuwa vyombo hivyo vitasaidia katika usimamizi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kuendeleza mradi wa Faiba Mlangoni Kwako.

Pia amesema vitachangia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja wa TTCL kote nchini.

Kwa mujibu wa Marwa, shirika linatarajia kupokea magari mengine matano ifikapo mwishoni mwa Mei 2026 ili kuendelea kuboresha shughuli za masoko na mauzo.

Amesisitiza kuwa magari hayo yatakuwa chachu ya kusimamia kwa ufanisi miundombinu ya mawasiliano, hususan Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao ni mhimili mkuu wa ujenzi wa Tanzania ya kidigitali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com