Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI, TGNP NA WADAU WAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA MOSHI

Na Deogratius Temba, Moshi

Serikali kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na wadau mbalimbali imeendelea kuimarisha mifumo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia (GBV), kupitia mafunzo maalum yanayolenga kuboresha uratibu, utekelezaji wa sheria na upatikanaji wa haki kwa wahanga.

Mafunzo hayo yanafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi chini ya mradi wa “Kuvunja Vikwazo – Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (GBV) na Kukuza Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu”, yakiwakutanisha wadau kutoka ngazi ya halmashauri hadi vijiji na mitaa. Washiriki wanajumuisha maafisa wa mahakama na ofisi ya mashtaka, polisi dawati la jinsia, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, wajumbe wa MTAKUWWA, viongozi wa dini na mila, pamoja na kamati za shule na zahanati na watoa huduma za afya.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwezeshaji Deogratius Temba alisema ushirikiano kati ya Serikali, TGNP na wadau ndiyo msingi wa mafanikio katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. “Tunapojenga uwezo wa wadau hawa kwa pamoja, tunaimarisha mifumo ya kitaifa na ya kijamii inayohakikisha matukio ya ukatili yanazuiwa, yanaripotiwa kwa wakati na kushughulikiwa ipasavyo,” alisema.

Aliongeza kuwa juhudi hizo zinaunga mkono utekelezaji wa mikakati ya kitaifa na kimataifa ikiwemo Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II)  pamoja na mifumo mingine, ambayo inalenga kuhakikisha huduma zinawafikia wahanga kwa ufanisi katika ngazi zote.

Katika mafunzo hayo, msisitizo umewekwa katika ujenzi wa “nguvu ya pamoja” miongoni mwa wadau, kuimarisha mnyororo wa kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia, na kuhakikisha kesi hizo zinafikia mwisho kwa haki kupatikana. Washiriki pia wanajengewa uwezo wa kuandaa mipango ya vitendo itakayotekelezwa katika maeneo yao.

Mratibu wa Dawati la Jinsia wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, SP Asia Matauka, alisema pamoja na maboresho ya mifumo hiyo, bado changamoto ya upatikanaji wa ushahidi kwa wakati inaendelea kujitokeza. “Baadhi ya wahanga huchelewa kutoa taarifa, na wakati mwingine familia hujaribu kumaliza kesi nyumbani kupitia wazee wa mila, jambo linalodhoofisha mchakato wa haki,” alisema.

Kwa upande wake, Isaack Daud Laizer, mzee wa mila kutoka kata ya Mabogini, alisema jamii imeanza kuchukua jukumu la moja kwa moja katika kupambana na ukatili wa kijinsia. Alieleza kuwa viongozi wa mila wameweka mikakati ya kuelimisha jamii, hususan vijana, ili kukomesha vitendo kama ukeketaji, ndoa za utotoni na ubakaji, pamoja na kulinda haki ya watoto wa kike kupata elimu.

Uchambuzi unaonyesha kuwa juhudi hizi za pamoja kati ya Serikali, TGNP na wadau zinasaidia kuboresha mifumo ya rufaa na uratibu wa huduma kwa wahanga, huku zikiongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria. Hii inachangia kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hayabaki kuwa ya sera pekee, bali yanatekelezwa kwa vitendo katika jamii.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yanaashiria hatua muhimu katika kuimarisha mifumo jumuishi na shirikishi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, na kuweka msingi imara wa jamii salama, yenye usawa na inayozingatia haki za binadamu.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com