
Wananchi wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wamewaomba viongozi kuhakikisha tamasha la utalii la Same Utalii Festival linafanyika kila mwaka kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa jamii.
Wito huo umetolewa leo na kina mama lishe wakati wa joggin ya kuhamasisha tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Aprili 10 hadi 12 mwaka huu, likiwa ni msimu wa tatu tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza katika joggin hiyo, Anna Mzava, ambaye ni mama lishe katika stendi ya mabasi wilayani Same, alisema tamasha hilo limekuwa msaada mkubwa kwao kiuchumi.

Alisema mbali na kuhamasisha utalii, tamasha hilo limeongeza kipato kwa wafanyabiashara wadogo kutokana na ongezeko la watu wanaohudhuria.
“Tunaomba tamasha hili liwe endelevu kwani sisi wananchi wa chini tunafaidika nalo. Biashara zetu zinaenda vizuri na tunapata fedha zaidi. Kwa mfano, badala ya kupika mchele kilo tatu, wakati wa tamasha napika hadi kilo 10 na zote zinaisha,” alisema Mzava.
Kwa upande wake, Jumanne Idd alisema tamasha hilo limekuwa chachu ya kutangaza utalii wa wilaya ya Same pamoja na vyakula vya asili vya kabila la Wapare.
Aliongeza kuwa tukio hilo limechangia kuitangaza wilaya hiyo kitaifa na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi wakati wa msimu wa tamasha.
Akizungumza katika joggin hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande, alisema wamejipanga kuhakikisha tamasha hilo linakuwa endelevu ili kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.
Alisema halmashauri itaendelea kubuni na kuibua vivutio vipya ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
“Faida kubwa tunazotarajia ni za kiuchumi.Panapokusanyika watu wengi ni fursa, kwani wanahitaji huduma mbalimbali na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi,” alisema Mapande.
Social Plugin