Mwanasiasa na mwanadiplomasia wa kimataifa, Gertrude Mongela, amesema dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto ya migogoro ya kizazi kati ya wazee na vijana inayosababishwa na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na teknolojia.Mongela amesema suluhisho si lawama bali ni majadiliano ya wazi na ya heshima kati ya pande zote ili kujenga mshikamano na kupunguza sintofahamu.
Ameeleza kuwa mabadiliko ya maisha yameathiri malezi ya watoto na uhusiano wa kifamilia, tofauti na zamani ambapo kulikuwa na ukaribu mkubwa kati ya wazazi na watoto na nidhamu ilijengwa kwa misingi ya mamlaka ya baba.
Mongela amesisitiza kuwa vijana wa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa zaidi za maisha, hivyo jamii inapaswa kuwapa uelewa na msaada badala ya lawama.
Ameonya pia dhidi ya wazee kuwalaumu vijana pekee akisema changamoto hizo zinawagusa wote.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia busara na majukwaa ya kijamii kama makanisa, misikiti na Bunge katika kujadili masuala ya kitaifa kwa lengo la kujenga amani, umoja na maendeleo ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Social Plugin