Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHUNGAJI MWITA: WAKRISTO WAWE NGUZO YA AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO WA KITAIFA




Mchungaji wa Kanisa la AICT Kambarage Mkoani Shinyanga , Jonas Mwita, amewahimiza Wakristo kuwa mfano bora katika jamii kwa kulinda na kudumisha amani, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza na waumini, Mchungaji Mwita amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, huku akibainisha kuwa kila mwananchi ana jukumu la kushiriki kikamilifu katika kulinda utulivu uliopo.

Ameeleza kuwa vitendo vidogo vinavyofanywa na watu katika maisha ya kila siku vina mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa mshikamano wa jamii, akiwataka Wakristo kuwa makini katika kuchagua marafiki na kuepuka ushawishi wa ushauri mbaya unaoweza kuhatarisha amani.

“Jamii yenye watu wanaoishi kwa maadili mema na hofu ya Mungu huwa na msingi imara wa umoja, upendo na mshikamano,” amesema Mchungaji Mwita.

Aidha, amewahimiza waumini kuendelea kushikamana, kuheshimiana na kuzingatia maadili katika maisha yao ya kila siku, akieleza kuwa mshikamano wa kitaifa huanzia katika ngazi ya familia na jamii kabla ya kufikia taifa zima.

Mchungaji Mwita ametoa rai kwa Wakristo na Watanzania kwa ujumla kuwa walinzi wa amani kwa vitendo, ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na utulivu, umoja na mshikamano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com