Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HAYATI ASKOFU ALOYSIUS BALINA (ASKOFU WA JIMBO KATOLIKI LA SHINYANGA 1997-2012)


Na Dotto Kwilasa

Katika dunia inayosonga kwa kasi, mara nyingi tunasahau watu walioweka msingi wa kile tunachokiona leo.

Lakini ukweli unabaki kuwa, historia haiishi kwa sababu mhusika ameondoka inaendelea kuishi kupitia sisi tunaoikumbuka na kuisimulia.

Leo, kama mwandishi na kama sehemu ya jamii ya Ng'wamapalala, najikuta nikiwa na wajibu wa kumuenzi na kukumbusha taifa juu ya mchango wa hayati Askofu Aloysius Balina.

Alizaliwa tarehe 21 Juni 1945 katika kijiji cha Isoso, Ntunzu, Bariadi. Safari yake ya elimu ilimlea katika misingi ya nidhamu na utumishi kupitia Seminari ya Mt. Pius X Makoko, Musoma na St. Mary’s Nyegezi, Mwanza. Mnamo tarehe 25 Juni 1971, alipokea daraja takatifu la upadre akiwa na miaka 26 akiwa tayari ameanza safari ya maisha ya kujitoa kwa wengine.

Kuanzia mwaka 1971 hadi 1975, alihudumu katika parokia mbalimbali ikiwemo Buhangija, Shinyanga Mjini, Salawe, Bugisi na Malili. Hapa ndipo alipoanza kuonesha uongozi wa vitendo unaogusa maisha ya watu wa kawaida.

Miaka ya 1975 hadi 1983, akiwa Gombera wa Seminari ya Mt. Pius X Makoko, alionesha upekee wa uongozi kwa kuimarisha uchumi wa seminari hiyo. Chini ya uongozi wake, ilinunuliwa boti ya kisasa ya uvuvi MV Makoko iliyokuwa na thamani ya dola 250,000 na uwezo wa safari ndefu zaidi ya kilomita 1000.

Huu haukuwa tu ubunifu, bali ulikuwa ni uthibitisho wa maono yake ya kujitegemea. 

Katika kipindi hicho, alifanya kazi bega kwa bega na hayati Askofu Justin Samba, huku baadhi ya wanafunzi wake wakija kuwa viongozi wakubwa wa Kanisa kama Askofu Mkuu Renatus Nkwande.

Mwaka 1984 ulikuwa mwanzo wa hatua kubwa zaidi alipoteuliwa na Pope John Paul II kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Geita, na kuwekwa wakfu rasmi mwaka 1985 katika Basilica ya Mt. Petro, Roma.

Akiwa Geita, alijenga misingi imara ya kiroho na kielimu, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Seminari ndogo ya Sengerema na kulikuza jimbo hilo hadi kuwa na parokia tisa.

Mnamo mwaka 1997, alihamishiwa Jimbo Katoliki la Shinyanga, ambako alihudumu hadi kifo chake mwaka 2012.

Hapa ndipo alipoacha alama kubwa zaidi alianzisha seminari mbili (Mt. Gregory Sayusayu na Mt. Aloysius Gonzaga Shanwa), akaanzisha Radio Faraja FM kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu afya na maendeleo, na kulikuza jimbo kutoka kutokuwa na seminari hadi kuwa na parokia 26.

Zaidi ya uongozi wa kiroho, Askofu Balina alikuwa nguzo katika sekta ya afya. Alikuwa mwanzilishi na mwenyekiti wa kwanza wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa zaidi ya miongo miwili, mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Bugando, na kiongozi katika taasisi mbalimbali za afya. Pia alihudumu kama Kamishna wa TACAIDS kati ya mwaka 2002 hadi 2004.

Lakini zaidi ya vyeo na majukumu, alikumbukwa kwa kusimama upande wa haki akipinga kwa nguvu zote mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino, na alipigania elimu kwa wanawake akiamini kuwa maendeleo ya jamii hayawezi kupatikana bila usawa.

Alifariki tarehe 6 Novemba 2012 katika Hospitali ya Bugando, Mwanza.

Kifo chake kiliacha pengo kubwa, lakini urithi wake umeendelea kuishi katika taasisi, watu na mabadiliko aliyoyaanzisha.

Leo hii, tunapomkumbuka, hatufanyi hivyo kwa mazoea tunafanya hivyo kwa sababu ya kuenzi mchango wake, hatuna budi kuendelea kukumbushana kwamba maendeleo tunayoyaona leo yana mizizi yake kwa watu kama Askofu Balina.

Taarifa zilizotumika katika makala hii zimepatikana kupitia mchanganyiko wa
Nyaraka na kumbukumbu rasmi za Kanisa Katoliki (Jimbo la Geita na Shinyanga)
Machapisho na taarifa za Tanzania Episcopal Conference
Taarifa za taasisi za afya ikiwemo Bugando Medical Centre
Majadiliano na simulizi za waliowahi kufanya kazi na hayati Askofu Balina
Uzoefu binafsi na kumbukumbu za jamii (ikiwemo maeneo ya Ng'wamapalala na viunga vyake)

Kama wanajamii, tunawajibika kulinda na kusimulia historia hizi ili zisipotee, kwani ndani yake ndipo kuna dira ya kizazi kijacho.

Raha ya milele umpe Ee Bwana, na mwanga wa milele umwangazie. Apumzike kwa amani. Amina.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com