Na mwandishi wetu, Dar
Aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais mwaka 2025 kupitia chama cha NLD, Doyo Hassan, amewataka Watanzania kuacha mara moja tabia ya kuwatukana na kuwakejeli Wajumbe wa Tume ya Uchunguzi, akisisitiza kuwa hatua hiyo inakiuka misingi ya heshima, ustaarabu na maadili ya kitaifa.
Doyo amesema kuwa wajumbe wa tume hiyo ni watu wenye umri mkubwa, uzoefu mpana na waliobobea katika masuala ya kitaaluma na kimataifa, hivyo wanastahili kuheshimiwa badala ya kubezwa. Ameeleza kuwa michango yao inalenga kusaidia taifa kupata ukweli na suluhisho la changamoto zilizojitokeza, siyo kuwa chanzo cha migogoro mipya ya kijamii.
Amesisitiza kuwa mijadala ya kitaifa inapaswa kufanyika kwa hoja na si kwa lugha ya matusi au kejeli, akionya kuwa mwenendo huo unaweza kudhoofisha mshikamano wa kitaifa na kuharibu taswira ya nchi kimataifa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuwa na subira wakati wakisubiri matokeo ya kazi ya tume hiyo, huku akihimiza matumizi ya njia za kistaarabu kutoa maoni na hoja. Kwa mujibu wa Doyo, kujenga taifa lenye misingi ya haki na uwajibikaji kunahitaji pia nidhamu ya mawasiliano na kuheshimiana miongoni mwa wananchi.
Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu ripoti na kazi za Tume ya Uchunguzi ukiendelea kushika kasi katika majukwaa mbalimbali ya kijamii na kisiasa nchini.

Social Plugin