Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DOYO: NINA MATUMAINI MAKUBWA NA TUME YA JAJI CHANDE



Na mwandishi wetu,Dar

Aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema ana matumaini makubwa na Tume ya Jaji Chande inayochunguza matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Doyo ameeleza kuwa matarajio yake yanatokana na muundo wa Tume hiyo, ambao umejumuisha wataalamu wenye uzoefu na weledi wa hali ya juu katika nyanja mbalimbali za uongozi na utumishi wa umma. 

Amesisitiza kuwa uwepo wa Majaji wastaafu ndani ya Tume hiyo unaipa uzito mkubwa katika kuhakikisha haki inatendeka na ukweli unabainishwa bila upendeleo.

Aidha, amebainisha kuwa kujumuishwa kwa Mawaziri wastaafu pamoja na viongozi wakuu wa zamani wa vyombo vya ulinzi na usalama kunatoa picha ya Tume yenye uwezo mpana wa kuchambua masuala ya kisiasa, kijamii na kiusalama kwa kina zaidi. Kwa mtazamo wake, mchanganyiko huo wa uzoefu unajenga msingi imara wa uchunguzi wenye tija.

Doyo amewatoa wasiwasi Watanzania kuwa wanapaswa kuwa na imani na mchakato unaoendelea, akieleza kuwa Tume hiyo ina kila sababu ya kutoa ripoti itakayozingatia ukweli wa matukio na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuepusha kujirudia kwa hali kama hiyo siku zijazo.

Amesisitiza umuhimu wa Tume hiyo kufanya kazi kwa uwazi, haki na weledi ili kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za nchi, huku akieleza matarajio yake kuwa matokeo ya uchunguzi huo yatakuwa na mchango chanya katika kudumisha amani na utulivu nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com