Na mwandishi wetu, Arusha
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameendelea kuwasisitiza Watanzania waendelee kudumisha amani nchini kwa sababu inawawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
“Tuwe makini na watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani kwa kuwa wengine walipwa kwa vitendo hivyo. Kama wao wamechagua maisha hayo wasiiuze nchi yetu. “Lazima tulinde amani ya nchi yetu.”
Amesema wanufaika wa kwanza wa amani ni wale wanaoishi katika eneo husika, hivyo hawana budi kuendelea kulinda amani na umoja wa kitaifa ili waendeleze shughuli mbalimbali za maendeleo.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Aprili 17, 2026) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kona ya Mbauda akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri Mkuu amesisitiza hayo mara baada ya kukagua barabara ya Kilombero-Mbauda-Kisongo na Mbauda Losinyai zinazojengwa kwa njia nne pamoja na kuwekewa taa.
Ujenzi wa barabara hizo zenye jumla ya urefu wa kilomita 13 ni miongoni mwa maandalizi ya Mashindano ya Mpira wa Miguu ya Mataifa ya Afrika (AFCON), 2027 ambapo Tanzania ni mwenyeji.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema kuwa ujenzi wa barabara hizo unakwenda kuwasaidia wananchi wa Arusha pamoja na Watanzania kwa ujumla, akimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha shilingi bilioni 27 ambapo kati yake bilioni 17 ni kwaajili ya mkandarasi na Shilingi bilioni 10 ni za fidia kwa waliopisha mradi huo.



Social Plugin