Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MTATIRO AAGIZA UKARABATI WA BARABARA YA ILOLA UKAMILIKE HARAKA KUONDOA ADHA

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza baada ya kukagua barabara ya Ilola ambayo iliharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha,baada ya diwani wa Kata ya Ilola Kisena Fred kutoa taarifa ya barabara hiyo.

       Na Stella Herman, Shinyanga

 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro  amesema hakuna nafasi ya visingizio pale dharura zinapotokea hasa katika kipindi hiki cha masika ili kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya miundombinu ya barabara.

Mtatiro ametoa kauli hiyo usiku alipofika kukagua utekelezaji wa maagizo ya serikali katika eneo korofi la barabara ya Didia–Solwa upande wa Kata ya Ilola,ambapo amesisitiza kuwa hatua za haraka zimechukuliwa  ili kuhakikisha wananchi wanapita bila usumbufu.

“Nimefika hapa usiku huu kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya serikali kuhakikisha barabara hii inakamilika haraka na namshukuru sana Mhe diwani Kisena kwa kusimamia suala hili” amesema

Ameonya kuwa si jambo linalokubalika kwa miundombinu iliyopata dharura kusubiri kwa muda mrefu kupata bajeti, amesema hatua za dharura zinapaswa kuchukuliwa mapema ili kuzuia madhara makubwa zaidi.

Mtatiro amebainisha kuwa kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita mbili kilikuwa katika hali mbaya na kingeweza kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya maeneo ya Solwa na Didia endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.

Amempongeza Diwani wa Kata ya Ilola, Kisena, kwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu changamoto hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo imewezesha serikali kuingilia kati kwa haraka na kuwanusuru wananchi na wafanyabiashara waliokuwa hatarini kushindwa kupitisha mazao yao.

Aidha, alimuelekeza mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi inakamilika ifikapo Aprili 10, 2026 ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwa wananchi.

Meneja wa TARURA Mhandisi Samson pamphil amesema barabara ya Didia–Solwa yenye urefu wa kilomita 55.3 ilikuwa imeharibika vibaya kufuatia mvua za masika  hali iliyosababisha kutokea kwa madimbwi makubwa na mashimo yaliyokuwa yanahatarisha usalama wa watumiaji.


Diwani wa Kata ya Ilola Kisena Fred akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara.

Kutokana na hali hiyo, wananchi walikuwa wakipata ugumu wa kupita, huku baadhi ya wanafunzi wakishindwa kupita hadi wapate msaada wa  kuwavusha  kama ilivyotokea kwa diwani wa Kata ya Ilola Kisena Fred  ambaye wakati imetokea changamoto hiyo alikutana na watoto na kuwavusha kwa kutumia pikipiki.

Changamoto hiyo ilibainika Februari 19, 2026, na baada ya kuripotiwa kwa mamlaka husika, hatua za haraka zilichukuliwa ikiwemo kumtumia mkandarasi aliyekuwa akifanya kazi Kata ya Lyabukande kushughulikia eneo hilo lililokuwa na uhitaji wa dharura.

Wananchi wa Kata ya Ilola wameishukuru serikali ya Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua za haraka kurekebisha barabara hiyo, wakisema imekuwa mkombozi mkubwa kwao na imeondoa adha waliokuwa wakikabiliana nayo kwa muda.

“Kweli serikali ya Mama Samia imesikia kilio chetu, hatua zimechukuliwa haraka na sasa tunaanza kuona matokeo,” walisema baadhi ya wananchi.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza usiku baada ya kufika kukagua barabara ya Ilola
Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Ilola



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com