Na mwandishi wetu,Dar
Mchambuzi wa masuala ya amani na maendeleo Dkt. Said Jafo amesisitiza umuhimu wa kuheshimu na kutambua mchango wa amani katika maendeleo na ustawi wa jamii na mwananchi mmoja mmoja, akitoa rai kwa kila Mtanzania bila kujali nafasi yake kuwajibika katika kuhakikisha anailinda amani na kudhibiti vihatarishi vinavyodhohofisha amani nchini
Dkt. Jafo amebainisha hayo katika mahojiano maalumu aliyoyafanya na chombo kimoja cha habari Jijini Dar Es Salaam leo Alhamisi Aprili 02, 2026, akibainisha kuwa msisitizo unaotolewa na Viongozi wa serikali kuhusu amani ni suala muhimu ambalo linapaswa kuzingatiwa kwa kufikiri zaidi kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza pale amani inapotoweka.
"Ukimsikia mtu anazungumzia amani usibeze, hii amani ni hitaji la kila mtu, tajiri anahitaji amani, maskini anahitaji amani, Kiongozi, raia, mwanasiasa na hata mtu wa dini kila mtu anahitaji amani. Tunapowasikia viongozi wa nchi wanapozungumzia amani tafakuri inatuambia una macho ya kuona na masikio ya kusikia sasa wao bila shaka wanaogopa madhara yatakayowakuta raia wao pale amani inapotoweka." Amesema Dkt. Jafo.
Dkt. Jafo ameendelea kusema kuwa amani huwezesha shughuli za kiuchumi, kijamii, na kielimu kustawi bila hofu, huku ikijenga upendo, mshikamano, na kuimarisha utawala wa sheria, akisisitiza kuwa jamii yenye amani hupunguza migogoro, msongo wa mawazo, na kuwezesha maisha bora ya kila siku.
Jafo anaungana na wachambuzi wengine wa siasa na uchumi ambao wamesisitiza kuwa umuhimu wa amani unajumuisha pia kukuza Maendeleo ya Kiuchumi kwa kuruhusu watu kufanya shughuli za uzalishaji mali, biashara, na uwekezaji bila hofu ya uharibifu.
Baadhi ya wanasaikolojia pia akiwemo Bw. Richard Kisaka amenukuliwa akisema kuwa kwa kuondoa hofu na vurugu, amani hupunguza msongo wa mawazo na kuleta utulivu wa nafsi suala ambalo limekuwa likisaidia mtu binafsi, familia na jamii kustawi.

Social Plugin