Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AANGUKIA MIKONONI MWA POLISI NA MALI ZA WIZI




Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Marco Chilya akiwa ameshika sare za Jeshi ambazo mtuhumiwa huyo alikua akizitumia wakati wa kutenda uhalifu wake Gari aina ya Toyota IST lenye namba T.829 DYH lililokamatwa wakati wa upekuzi uliofanyika nyumbani kwake mtuhumiwa huyo

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia Michael Ngonyani (38), mkazi wa Mtyangimbole, kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa uhalifu unaodaiwa kujumuisha wizi wa magari katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya.

Kukamatwa kwake kunatajwa kuwa mafanikio ya operesheni maalum ya polisi iliyolenga kuwabaini wahalifu wanaojificha kwa mbinu zisizo za kawaida.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya, mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 31, 2026 katika eneo la Mtyangimbole, Halmashauri ya Madaba.

Baada ya upekuzi kufanyika nyumbani kwake, alikutwa akiwa na gari aina ya Toyota IST lenye namba T.829 DYH pamoja na leseni nne za udereva zenye majina tofauti, hali inayozua mashaka juu ya matumizi yake.

Aidha, upekuzi huo uliwezesha kupatikana kwa vifaa mbalimbali vinavyodhaniwa kuwa vya wizi, ikiwemo televisheni mbili za ukubwa wa inchi 65 na 55, sound bar moja aina ya Skywood pamoja na mashine ya kusukuma maji (water pump).

Polisi wanaamini mali hizo zinaweza kuwa zimepatikana kwa njia zisizo halali na zinaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kubaini wamiliki halali.

Katika hatua nyingine ya kushangaza, mtuhumiwa huyo pia alikutwa akiwa na sare za Jeshi la Polisi (kaki) pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), zikiwemo suruali na fulana.

Inadaiwa kuwa alizitumia kujifanya askari ili kurahisisha utekelezaji wa uhalifu wake.

Kamanda Chilya amesema uchunguzi unaendelea kubaini alivyopata sare hizo na hatua kali za kisheria zitachukuliwa mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com