

Na Mbuke Shilagi Kagera.
Katika hali ya kugusa mioyo na kuonesha mshikamano wa kijamii, wahitimu wa shule ya sekondari Kagemu wa mwaka 2008–2011 wametoa msaada wa Pasaka kwa watoto wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto cha Uyacho, kilichopo Hamugembe, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Vijana hao, ambao wameendelea kuwasiliana na kushikamana kupitia kundi lao la WhatsApp, wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kuendeleza shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kusaidia jamii inayowazunguka. Msaada huo umekuwa sehemu ya kuadhimisha sikukuu ya Pasaka kwa vitendo, kwa kuwapa faraja watoto hao pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu ya kila siku.
Katika msaada huo, wahitimu hao wamekabidhi kiasi cha kilo 50 za mchele na kilo 50 za sukari, pamoja na lita 10 za mafuta ya kupikia. Aidha, wametoa miche mitano ya sabuni na kuchangia umeme wenye thamani ya shilingi 50,000/= sawa na units 136 kwa matumizi ya kituo hicho.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, mmoja wa wanachama wa kundi hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Bukoba Mjini, James Michael Nyamanza, amesema kuwa kundi lao limekuwa na utaratibu wa kutoa misaada kila mwaka, hasa katika vipindi vya mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma.
"Kila mwaka ifikapo mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma, tumekuwa tukijitahidi kugusa maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kutoa mahitaji muhimu katika vituo mbalimbali. Hii ni sehemu ya wajibu wetu kwa jamii",amesema Nyamanza.
Social Plugin