Na Hadija Bagasha - Tanga
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abrahman Abdallah, wakati wa ziara yake ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa hivi karibuni katika Soko la Mgandini, jijini Tanga, kuhusu kuboresha usafi na mazingira ya soko hilo.
Mwenyekiti Rajab amesema baadhi ya viongozi wamekuwa na tabia ya kulalamika badala ya kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi, hali inayosababisha wananchi kukosa imani na kushindwa kupata msaada wa haraka kwenye kero zao.
Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo, badala ya kuwa chanzo cha kuongeza malalamiko, akieleza kuwa CCM inahitaji viongozi wa vitendo na wenye uwajibikaji.
“Hatuhitaji viongozi wa kulalamika, tunahitaji viongozi wanaochukua hatua kutatua changamoto za wananchi. Mlichokifanya ni kutimiza wajibu wenu,” amesema Rajab.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha maeneo ya kukusanyia taka ndani ya soko hilo yanaboreshwa kwa kujazwa kifusi, pamoja na kurekebisha barabara za ndani ili kurahisisha shughuli za usafi na kudhibiti athari za mazingira.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha maji ya mvua yanaelekezwa vizuri kwenye mifereji, ili kuepusha mafuriko yanayoweza kuharibu miundombinu na kuongeza uchafu katika maeneo ya biashara.
Awali, wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya usafi na miundombinu ya vyoo katika soko hilo, Mwenyekiti Rajab alionesha kutoridhishwa na mazingira ya Mgandini na kutoa muda wa mwezi mmoja kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha hali ya usafi inaboreshwa.
Baada ya kufanya ziara ya ufuatiliaji, Rajab aliwapongeza Mstahiki Meya pamoja na viongozi wa Jiji kwa kuanza kuchukua hatua za utekelezaji wa maagizo hayo, akieleza kuwa hali ya uchafu iliyokuwepo awali haikuwafurahisha viongozi wala wafanyabiashara.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ameonya kuwa hataki kusikia visingizio, bali anataka kuona utekelezaji wa vitendo ukiendelea kwa kasi.
“Ndani ya mwezi mmoja kuanzia Aprili 9 hadi Mei 9, tunatarajia kuona kazi imeanza. Hatutaki hadithi, tunataka vitendo,” alisisitiza.
Akijibu maelekezo hayo, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Selebos Mustafa, amesema Halmashauri tayari imeanza kuchukua hatua mahsusi za kuboresha hali ya usafi katika soko hilo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha maeneo ya ukusanyaji taka na kuongeza ufuatiliaji wa kila siku.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwanzange, Khalidi Rashid, amesema kucheleweshwa kwa fedha za mapato kuwasilishwa kwenye halmashauri kumechangia changamoto ya usafi katika soko hilo, lakini ameeleza kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kurejesha hali ya usafi na mazingira bora kwa wafanyabiashara.
Ziara ya Mwenyekiti Rajab imeelezwa kuwa ni sehemu ya msukumo kwa viongozi wa serikali za mitaa na halmashauri kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutatua kero za wananchi kwa wakati.
Ziara hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kuhusu kuboresha usafi katika soko la Mgandini, ambapo hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuondoa uchafu uliokuwepo awali na kuimarisha usimamizi wa mazingira ya soko.











Social Plugin