Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAHABARI WAKUMBUSHWA WAJIBU WA KULINDA AMANI WAKATI WA MIGOGORO


Meneja Kitengo cha Hudumaza Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Mhandisi Andrew Kisaka akiwasilisha mada kuhusu utangazaji wakati wa migogoro kwenye kikao cha wadau wa sekta ya habari kilicholenga kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kuhamasisha amani, utulivu, umoja wa kitaifa na maridhiano nchini.
Meneja Kitengo cha Hudumaza Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Mhandisi Andrew Kisaka akiwasilisha mada kuhusu utangazaji wakati wa migogoro.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kutumia nafasi yake kwa uangalifu mkubwa wakati wa kuripoti migogoro, kwa lengo la kuhamasisha amani, utulivu, umoja wa kitaifa na maridhiano badala ya kuchochea mivutano katika jamii.

Wito huo umetolewa Aprili 17, 2026 na Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, wakati akiwasilisha mada kuhusu utangazaji wakati wa migogoro kwenye kikao cha wadau wa sekta ya habari kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari – Maelezo.

Kikao hicho kililenga kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kuhamasisha amani, utulivu, umoja wa kitaifa na maridhiano nchini.

Kisaka alieleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuathiri mitazamo ya jamii, hivyo vinapaswa kuhakikisha taarifa wanazotoa zinazingatia ukweli, usawa na uwajibikaji bila upendeleo, hasa katika nyakati za migogoro.

Alisema matumizi ya lugha ya kichochezi au kuripoti kwa mihemko yanaweza kuongeza taharuki na kuharibu jitihada za kujenga amani.

Badala yake, wanahabari wanapaswa kuandika na kutangaza habari kwa weledi, wakilenga kupunguza mvutano na kuhamasisha maelewano miongoni mwa wananchi.

Aidha, alibainisha kuwa vyombo vya habari vinapaswa kutoa nafasi kwa pande zote zinazohusika katika migogoro kusikika kwa usawa, huku vikihimiza suluhisho la amani na maridhiano, jambo linalochangia kuimarisha umoja wa kitaifa.

“Vyombo vya habari vinaweza kuwa sehemu ya tatizo au sehemu ya suluhisho. Ni muhimu vitumie nafasi yake kujenga daraja la maelewano na si kuongeza mgawanyiko,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Kisaka, uandishi wa habari unaozingatia maadili katika mazingira ya migogoro unapaswa kulinda utu wa binadamu, kuepuka maudhui yanayoweza kudhalilisha wahusika, na kuhakikisha taarifa zinachangia utulivu wa jamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Maelezo, Zamaradi Kawawa, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema lengo kuu ni kuwajengea uelewa wadau wa sekta ya habari kuhusu wajibu wao katika kulinda na kuimarisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa kupitia kazi zao za kila siku.

Aliwataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao hasa katika vipindi vya migogoro, akisisitiza umuhimu wa kuandika habari zenye kujenga mshikamano wa kitaifa.

“Wakati wa migogoro, sisi waandishi wa habari tunatakiwa kuandika habari za kujenga. Tunapaswa kuhamasisha amani, utulivu, umoja wa kitaifa na maridhiano nchini. Hakikisheni mnaandika habari zinazowaunganisha Watanzania, si zinazobomoa taifa,” alisema Kawawa.

Washiriki wa kikao hicho walijumuisha viongozi na wanachama kutoka Tanzania Bloggers Network (TBN), JUMIKITA (Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania) pamoja na TADIO (Mtandao wa Redio za Kijamii Tanzania).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com