
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akionesha tuzo aliyokabidhiwa kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza vipaji na kuendeleza Mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu wilayani Kondoa. Tuzo hiyo imetolewa na Ofisi ya Mbunge wakati wa mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu yaliyofanyika katika kijiji cha Bukulu, Wilayani Kondoa mkoani Dodoma Machi 7, 2026.Katika kilele cha mashindano ya kuhifadhi Kurani wilayani Kondoa mkoani Dodoma, hali ya kiroho na utulivu ilitawala huku sauti ya Serikali ikisikika kwa msisitizo kuhusu mustakabali wa taifa.
Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, alitumia jukwaa hilo kutoa mwito mzito kwa wananchi, akiwataka kutumia msimu huu wa mfungo na sikukuu zinazokaribia kama muda wa toba, upendo, na kuiombea nchi pamoja na Rais.
Dk. Mwigulu alieleza kuwa sifa ya Tanzania kama "kisiwa cha amani" na kimbilio la wengi si jambo la kupuuza, bali ni urithi unaopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Alibainisha kuwa siri ya kupunguza kero na changamoto nyingi ambazo Serikali inapambana nazo kila siku inategemea jambo moja kuu: maadili na ibada. Alisisitiza kuwa jamii ikijengwa katika misingi ya kumcha Mungu, nidhamu na uadilifu vitazaliwa kiasili.
Msisitizo mkubwa wa Waziri Mkuu ulihamia kwenye ombwe la malezi. Alifafanua kuwa malezi ya mtoto ni mchakato wa hatua kwa hatua, akitolea mfano wa jinsi mtoto anavyofundishwa neno moja baada ya jingine hadi anapoweza kuongea, au anavyoshikwa mkono kidogo kidogo hadi anapoweza kutembea mwenyewe.
Dk. Mwigulu alionya kuwa usipomfundisha mtoto kuwa mcha Mungu tangu akiwa mdogo, ni vigumu kumubadilisha ukubwani. Alitoa rai kwa wazazi, walezi, na walimu wa Kurani kuhakikisha kuwa kile kinachohifadhiwa vichwani mwa vijana kinaishi katika vitendo vyao vya kila siku.
Katika kuitambua nafasi ya taasisi za dini, Waziri Mkuu alihakikisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zote za madhehebu zinazolenga kuleta manufaa kwa jamii.
Social Plugin