Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAJUMBE WA KAMATI YA JPCDS WAJIONEA MAAJABU YA HIFADHI YA NGORONGORO



Wajumbe wa Kamati ya Wataalamu wa Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama (Joint Permanent Commission of Defense and Security – JPCDS) kutoka Tanzania na Zambia, wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Jacob Jack Mwiimbu Februari 26, 2026 walipata fursa ya kutembelea na kujionea maajabu ya Hifadhi ya Ngorongoro wakati wakishiriki kikao cha siku tano Jijini Arusha kilicholenga kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka na matishio yanayoibukia.

Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa kulinda rasilimali za asili kama sehemu ya ajenda ya usalama wa kikanda.

Kote duniani inafahamika kuwa, Ngorongoro ni hifadhi ya kipekee duniani, iliyotokana na kaldera bonde kubwa la volkano lililosababishwa na mlipuko na kuporomoka kwa volkano kubwa takribani miaka milioni 2 hadi 3 iliyopita.

 Ambapo unapoteremka ndani ya kreta yake, unashuka hadi kina cha takribani mita 600 na kujikuta katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 260, likiwa limezungukwa na kuta za asili zinazovutia na kuhifadhi mfumo wake wa ikolojia.

Aidha, wakiwa ndani ya kreta hiyo, wajumbe hao waliona mandhari ya kuvutia ya nyanda pana za majani, misitu midogo na mabwawa ya maji, likiwemo bwawa la chumvi maarufu kama Lake Magadi. 

Upekee wa eneo hili unalifanya kuwa kreta kamili na kubwa zaidi duniani isiyojaa maji wala kuvujisha maji, huku ikiwa na mkusanyiko mkubwa wa wanyamapori wanaoishi kwa kudumu ndani yake.

Maajabu ya Ngorongoro hayaishii kwenye mandhari na wanyamapori pekee. Eneo hili ni miongoni mwa hifadhi chache duniani ambapo binadamu, hususani jamii ya Wamasai wanaishi kisheria na kuchunga mifugo yao sambamba na wanyamapori.

Itakumbukwa kuwa, Mwaka 1959 eneo hilo lilitengwa rasmi kama hifadhi mchanganyiko ya wanyamapori na makazi ya watu na mwaka 1979 likatangazwa kuwa Urithi wa Dunia na UNESCO kutokana na thamani yake ya kipekee ya asili na kihistoria.

Vilevile, hifadhi ya Ngorongoro iko karibu na Olduvai Gorge, eneo maarufu kama chimbuko la binadamu, lililotoa ushahidi muhimu wa kale kuhusu historia ya mwanadamu. Hivyo, pamoja na kuwa kivutio cha utalii, pia ni hazina ya tafiti za kisayansi na urithi wa kihistoria wa dunia.

Kutokana na wingi na utofauti wa wanyamapori, wataalamu hao wa sekta ya ulinzi na usalama walipata fursa ya kuona wanyama mbalimbali wakiwemo, tembo, simba, nyati, nyumbu, viboko, pundamilia, swala, digidigi, ngiri, mbweha, fisi na ndege wa aina mbalimbali. Uwepo wa wanyamapori hao kwa wingi ndani ya kreta moja ni kielelezo cha mafanikio ya juhudi za uhifadhi zinazoendelea kufanywa na mamlaka husika.

Ziara hiyo imeongeza hamasa kwa wajumbe hao kuimarisha ushirikiano katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka, hususan uhalifu dhidi ya maliasili. Wametambua kuwa kulinda urithi wa kipekee tuliyo rithishwa katika mataifa yetu ni jukumu la pamoja kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, wakienzi maono ya waasisi wa mataifa yao, Julius Kambarage Nyerere na Kenneth Kaunda, waliothamini mshikamano wa kikanda na uhifadhi wa rasilimali za taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com