
Na Beda Msimbe
Katika kuelekea kilele cha uchumi wa kidijitali, ni dhahiri kuwa kasi ya teknolojia lazima iende sambamba na kasi ya uwajibikaji. Hata hivyo, uzoefu wangu wa siku nne zilizopita na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kupitia huduma zao za T-Pesa na Faiba Mlangoni, umechora picha tofauti; picha ya ubabaishaji wa wazi unaogharimu muda, fedha, na ufanisi wa kazi wa mteja.
Safari hii ya kutaabika ilianza Jumatano iliyopita baada ya kufanya malipo ya shilingi 55,000 kwa ajili ya huduma ya intaneti ya Faiba nyumbani kwangu, Goba. Licha ya fedha kukatwa katika akaunti yangu ya T-Pesa, hakuna muamala wowote uliofika upande wa huduma ya Faiba, na akaunti yangu ikabaki gizani. Nililazimika kusafiri kutoka Goba hadi Posta kutafuta ufumbuzi, ambapo maofisa walithibitisha kuonekana kwa fedha hizo na namba ya malipo (control number), lakini walishindwa kukamilisha muamala huo kwa saa mbili, huku wakiniahidi kuwa tatizo lingeshughulikiwa.
Ahadi hiyo imekuwa wimbo wa kila siku usio na mwisho. Kuanzia Alhamisi hadi leo Jumamosi, nimekuwa nikipigwa kalenda na vituo vya huduma kwa wateja (Call Center). Nimepewa ahadi za kusubiri saa 24, ambazo baadaye ziligeuka kuwa saa 72, huku kila nikipiga simu nikijibiwa neno lile lile: "Tatizo lako linashughulikiwa." Swali la msingi hapa ni je, unashughulikiaje tatizo la muamala wa ndani wa shirika lile lile kwa zaidi ya saa 96?
Inasikitisha kuona kuwa T-Pesa ni ya TTCL, na Faiba ni ya TTCL, na bado mifumo hii miwili imeshindwa kuwasiliana ili kumhudumia mteja aliyelipia huduma. Matokeo yake, kifurushi namba 822627186 kimebaki bila mawasiliano kwa siku nne sasa. Hii si tu inakwaza utendaji kazi wangu unaotegemea intaneti, bali inatia doa juhudi za serikali katika kuimarisha TEHAMA na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika shirika hili la umma.
Hali hii inajenga picha mbaya kwa mashirika ya umma. Inakuwaje huduma ya kujiunga na vifurushi inatangazwa vizuri kwenye menyu lakini utekelezaji wake unakuwa wa kusua-sua hadi mteja alazimike kupiga "misele" ya kilomita kadhaa kufuata huduma? Inakuwaje mawakala wengi wa T-Pesa wanakata tamaa na kuacha kutoa huduma kwa sababu ya changamoto za kimfumo, kisha shirika likakaa kimya?
Kama uchumi wa kidijitali ndio mwelekeo wetu, basi TTCL wanapaswa kubadilika. Haingii akilini mteja kuhangaika kiasi hiki kwa huduma aliyoliptia. Ni wakati sasa wa mamlaka zinazohusika, ikiwemo TCRA, kuingilia kati na kuona namna mifumo hii inavyoweza kuboreshwa ili kumlinda mteja. Vinginevyo, malalamiko ya wananchi kuwa mashirika ya umma hayawezi kutoa huduma bora yataendelea kuwa na mashiko, na pendekezo la kutaka usimamizi mkali zaidi au hata mabadiliko ya kimuundo katika uendeshaji wa mashirika haya yatakuwa na uhalali.
Social Plugin