Na Mwandishi Wetu Malunde 1 blog, Shinyanga
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imeandaa hafla ya Iftari iliyowakutanisha viongozi wa serikali, dini, wadau pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Machi 17,2026, Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Emmanuel Maro, ameeleza kuwa Iftar hiyo ni fursa muhimu ya kukuza mshikamano, upendo na maelewano miongoni mwa wadau wa maendeleo.
Maro amesema mwezi Mtukufu wa Ramadhan unawakumbusha Watanzania umuhimu wa uvumilivu, kusaidiana na kuzingatia maadili mema, na kuongeza kuwa TRA imeona ni vyema kuandaa Iftari hiyo ili kuendeleza uhusiano mzuri na walipakodi na wadau wake.
Amebainisha kuwa ushirikiano uliopo kati ya TRA na walipakodi umeendelea kuleta matokeo chanya, ambapo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, mkoa wa Shinyanga ulikusanya zaidi ya shilingi bilioni 24.7, sawa na asilimia 115 ya lengo lililowekwa.
“Ufanisi huu umetokana na kuongezeka kwa ulipaji kodi wa hiari, hali inayotokana na ushirikiano mzuri kati ya TRA na wadau wetu. Tunawashukuru sana walipakodi na kuwaomba waendelee kushirikiana nasi ili kuvuka malengo ya mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema Maro.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuelezea uzinduzi wa mfumo mpya wa usimamizi wa kodi za ndani wa IDRAS, unaorahisisha huduma mbalimbali za kikodi ikiwemo usajili wa walipakodi, uwasilishaji wa marejesho ya kodi, malipo ya kielektroniki na ufuatiliaji wa madeni ya kodi.
Maro amesisitiza kuwa TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi, kuboresha huduma kwa wateja na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha biashara kukua, huku akiwahimiza wananchi kutoa na kudai risiti ili kujenga uchumi imara wa taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mh. Julius Mtatiro, ameipongeza TRA kwa kuandaa hafla hiyo muhimu, akieleza kuwa inaongeza mshikamano na kuimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi.
Iftar hiyo imeambatana na dua pamoja na kushiriki futari kwa pamoja katika hali ya amani, upendo na mshikamano, ikiwa ni ishara ya umoja na ushirikiano katika kujenga taifa lenye maendeleo.























































































Social Plugin