Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YALENGA KUBORESHA UCHUMI KUPITIA UJENZI WA LAMI BARABARA YA KOLANDOTO-MWANGONGO- KISHAPU


Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdalla Ulega akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 16, 2026 baada ya ukaguzi wa barabara ya Kolandoto–Mwangongo yenye urefu wa kilomita 52 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.


Na Sumai Salum- Kishapu

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdalla Ulega amekagua barabara ya Kolandoto–Mwangongo yenye urefu wa kilomita 52, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami.


Akizungumza na wananchi wa Kishapu baada ya ukaguzi huo uliofanyika Machi 16, 2026 jirani na Hoteli ya Kali, Mhunze, Waziri Ulega amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo uko kwenye mpango wa maendeleo na utawasilishwa katika Bunge la Bajeti litakaloanza hivi karibuni.


Amesema kupitia vikao vya bajeti, mradi huo utapatiwa kibali na kuanza mchakato wa kumpata mkandarasi atakayetekeleza ujenzi wake.


“Kupitia vikao vijavyo vya bajeti, mradi huu utapatiwa kibali na kutafutiwa mkandarasi ili ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, barabara hii iwe imekamilika,” amesema Ulega.


Aidha, amesema barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa kwani ikikamilika itarahisisha shughuli za uzalishaji na biashara kwa wananchi wa eneo hilo.


Amefafanua kuwa barabara hiyo itawasaidia wakulima, wafugaji, wafanyabiashara pamoja na wananchi wengine kupata unafuu wa usafiri na usafirishaji wa mazao, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya na elimu.


Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amewapongeza wananchi wa Kishapu kwa ushirikiano wao katika kupisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo mradi wa umeme wa jua unaotekelezwa katika eneo hilo, ambao unatarajiwa kunufaisha Watanzania wengi.


Pamoja na hayo, amewahimiza wananchi kuendelea kuwaombea viongozi wa Taifa na kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa taasisi za dini kuendelea kuhubiri amani na kuepuka ubaguzi ili kudumisha mshikamano katika jamii.


Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Lucy Mayenga na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi wamempongeza Waziri huyo kwa ujio wake kwani umetangaza neema na kuwapa matumaini mapya wananchi wa Kishapu ikiwa barabara hilo limekuwa ni kilio cha wananchi cha muda mrefu.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Lucy Mayenga akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Machi 16, 2026, kufuatia ziara ya Waziri wa Ujenzi kukagua barabara ya Kolandoto–Mwangongo yenye urefu wa kilomita 52 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Wakili, Julius Mtatiro akifuatilia Mkutano wa hadhara wa Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdalla ulega kizungumza na wananchi baada ya ukaguzi wa barabara ya Kolandoto- Mwangongo yenye urefu wa kilomita 52 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 16, 2026 kufuatia ukaguzi wa barabara ya Kolandoto–Mwangongo yenye urefu wa kilomita 52 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami



























Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com