Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James
Na Mwamvita Issa - Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesisitiza kuwa ili kujenga taifa lenye maendeleo endelevu na uwazi, sekta ya habari inapaswa kupewa nafasi ya kipekee katika mchakato wa maendeleo.
Mhe. James ametoa kauli hiyo leo Machi 17, 2026 wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Habari, Wahariri na Waandishi wa Habari (MISA TAN SUMMIT 2026), lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Akizungumza katika kongamano hilo, amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhabarisha na kuelimisha jamii, sambamba na kuchochea mijadala yenye tija kuhusu maendeleo ya taifa. Aliwahimiza waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuleta mabadiliko chanya kwa kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utawala.
Mhe. James amebainisha kuwa Mkoa wa Iringa una rasilimali nyingi zinazoweza kukuza uchumi wa taifa, zikiwemo sekta za kilimo, mifugo, misitu na utalii.
Ametaja vivutio vikubwa vya utalii kama Hifadhi za Taifa za Ruaha na Udzungwa, akieleza kuwa mkoa huo una nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha utalii katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, miundombinu, maji, nishati na utalii, huku akisisitiza kuwa uchumi wa mkoa huo unaendelea kukua kwa kasi.
Amewataka wahariri na waandishi wa habari kuitangaza Iringa ili kuvutia wawekezaji zaidi.
MISA Tanzania Yalenga Uandishi wa Habari wa Suluhisho
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema kongamano hilo lina lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wadau wa maendeleo.
Amewataka waandishi wa habari kuzingatia weledi na maadili ya taaluma, pamoja na kuandika habari zinazotoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili jamii.
Soko amefafanua kuwa MISA Tanzania ina mpango wa kuanzisha kituo maalum cha kusambaza taarifa za maendeleo kwa wananchi, ili kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika masuala ya maendeleo.
“Tunataka kutoa taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa njia itakayowafaidi moja kwa moja”,amesema.
Serikali Kushirikiana na MISA Tanzania
Mhe. Kheri James amekubali ombi la MISA Tanzania la kuanzisha kituo hicho, na kuahidi kuwa Serikali ya Mkoa wa Iringa itashirikiana kuhakikisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi unafanikiwa.
Kongamano hilo limeelezwa kuwa na mafanikio makubwa, likiwa limehamasisha umuhimu wa vyombo vya habari katika kuchochea maendeleo endelevu.
Ushirikiano kati ya sekta ya habari na wadau wa maendeleo umeelezwa kuwa nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye uwazi, uwajibikaji na ustawi wa kiuchumi.


Social Plugin