Safari yangu haikuwa fupi; ilikuwa ni safari ya kilometa 2,168 nikizunguka katika vumbi, lami, na kokoto. Kuanzia makao makuu ya nchi, Dodoma, nikapenya kuelekea Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza, nikashuka hadi nyanda za juu kusini mkoani Rukwa, kabla ya kurejea tena Dodoma. Dhamira ilikuwa moja tu: kushuhudia kwa macho na kuandika kwa kalamu yangu kile kinachofanyika katika kuwezesha vijana wa Kitanzania kujiajiri na kujiimarisha katika utaalamu walionao.
Nikizitafakari kilometa hizo, nimejionea mabadiliko makubwa ambayo, katika miaka 10 ijayo, yatalipatia Taifa letu nguvukazi yenye ujuzi stahiki kwa ajira endelevu. Kila mkoa niliopita, ujumbe ni mmoja: Serikali imeweka bayana dhamira yake ya kupunguza pengo la ujuzi linalowakabili vijana wengi nchini kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi na Uanagenzi. Kinachopaswa sasa ni vijana wenyewe kutumia uwezeshaji huu kujinoa na kuwa tayari kwa ushindani wa soko la ajira linalobadilika kila siku.
Katika vumbi na jasho la safari hiyo, kitu kimoja kilinigusa zaidi; kuona kundi kubwa la wasichana ambao wamepania kabisa kubadili mwelekeo wa maisha yao. Nilikutana na mabinti jasiri ambao wameamua kuachana na dhana potofu za kijinsia na kujiingiza kwa kichwa kwenye fani ngumu za ufundi. Nilishuhudia wasichana wakijifua kwa umahiri mkubwa katika ufundi wa magari, ufungaji wa mifumo ya umeme, teknolojia ya habari na mawasiliano (IT), ufugaji wa kisasa, pamoja na ufundi wa mabomba. Hawa si wasichana wanaosubiri ajira, bali ni mafundi na wataalamu wa kesho ambao wako tayari kuingia shambani na kwenye gereji kulijenga Taifa.
Mabadiliko haya ya kifikra na kiuchumi ndiyo kiini cha awamu ya nane ya programu hii iliyozinduliwa Machi 8, 2026, jijini Dodoma. Programu hii inakuja wakati muafaka ambapo nchi inajipanga kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ikihitaji nguvukazi yenye ushindani wa kimataifa. Katika awamu hii, Serikali imewekeza rasilimali nyingi kuwafikia vijana 5,746 nchi nzima kupitia vyuo 46 vilivyosambaa katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, vikiwemo vyuo vya sekta binafsi kama Chuo cha Laela kilichopo Sumbawanga na Pine cha Mwanza.
Simulizi ya "Sista" aliyenolewa na programu hii, akihama kutoka majukumu ya kiroho kanisani hadi kuwa mtaalamu wa kilimo shambani, ni ushahidi mwingine tosha wa namna programu hii inavyofungua milango ya fursa bila ubaguzi. Ni sehemu ya mikakati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu katika kuhakikisha kuwa nguvukazi ya Taifa inapata stadi muhimu za kuajirika au kujiajiri, hivyo kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi.
Sikuchoka kwa safari ile ndefu ya kilometa 2,168; kinyume chake, nilifurahi sana kuwa mmoja wa mashuhuda wa mabadiliko haya ya kihistoria. Kuona wasichana wakichafuka mikono kwa grisi ya magari na tope la shambani kwa ajili ya kutafuta ujuzi, kunanipa uhakika kuwa safari ya kuelekea mwaka 2050 inaongozwa na vijana wenye nia, nguvu, na maarifa ya kweli ya amali.
Social Plugin