
Mchambuzi wa masuala ya siasa na migogoro ya kimataifa, Dk Albanie Marcossy, ametoa darasa muhimu ambalo ni sharti kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake alielewe kwa kina.
Kupitia uchambuzi wake, Dk Marcossy ameweka wazi kuwa dhana tunazozisikia kila siku kama "Demokrasia, Haki za Binadamu, na Utawala Bora" mara nyingi hutumiwa na mataifa makubwa kama chambo cha kupumbaza mataifa yanayoendelea ili kufunika ajenda zao za siri za kiuchumi.
Huu ni ukweli mchungu unaopaswa kutufumbua macho wananchi kuwa, wakati wakubwa wanapiga kelele kuhusu haki, nyuma ya pazia wanapiga hesabu za jinsi ya kunufaika na rasilimali zetu.
Kwa kauli na tahadhari alizotoa mchambuzi huyo ni vyema Watanzania wakagundua kuwa amani na mshikamano wa taifa ndiyo ngao pekee iliyopo dhidi ya hila hizi za kimataifa.
Tunaposhuhudia watu kwenye mitandao ya kijamii wakijivika joho la "wanaharakati" na kupandikiza mbegu za chuki na kutoamini serikali, ni lazima tujiulize: Je, harakati hizi zinamnufaisha nani? Mara nyingi, sauti hizi hupata nguvu pale tunapokubali kulishwa uongo na kufuata mkumbo wa mihemko ya mtandaoni, bila kujua kuwa tunatumiwa kama madaraja ya kudhoofisha misingi ya nchi yetu kwa maslahi ya watu walio nje ya mipaka yetu.
Hivyo basi, wito mkubwa ni kwa wananchi kubaki na maslahi ya taifa . Tusikubali kuyumbishwa na kauli za mburukenge au vibaraka wanaofadhiliwa kuchafua taswira ya nchi yetu na kuleta taharuki.
Tunapaswa kuwa na akili ya kuchambua mambo na kuona kuwa utulivu wa Tanzania ndiyo rasilimali ghali kuliko zote. Wakati mataifa makubwa yakitafuta maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi, sisi jukumu letu la kwanza ni kulinda upendo, umoja, na amani tuliyorithishwa, tukikumbuka kuwa nchi ikivurugika, waathirika wa kwanza ni sisi wenyewe na si wale wanaopiga kelele wakiwa ughaibuni.
Social Plugin