Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAADILI YA NYERERE: SILAHA DHIDI YA CHUKI NA MIFARAKANO YA MITANDAONI




Katika kuelekea kilele cha miaka 104 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, msisitizo wa kurejea kwenye misingi ya uzalendo; umoja na mshikamano umepata msukumo mpya kama njia pekee ya kunusuru taifa dhidi ya wimbi la mahubiri ya chuki yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Marcelina Chijoriga, anabainisha kuwa mwenendo wa sasa wa baadhi ya watu kutumia majukwaa ya kidijitali kuchochea mifarakano inakiuka wazi misingi ya utu na usawa iliyowekwa na waasisi wa taifa hili, chini ya uongozi wa Rais wa kwanza wa taifa hili Julius Nyerere.

Mwalimu Nyerere, katika uhai wake, alipigania kwa dhati heshima ya mwanadamu na kukataa ubaguzi wa aina yoyote, akiamini kuwa amani ya kudumu inajengwa juu ya misingi ya uwajibikaji badala ya kutafuta umaarufu kupitia chuki.

Profesa Chijoriga anafafanua kuwa mshikamano wa kweli haupaswi kuwa na mipaka ya dini, kabila wala itikadi za vyama, bali unapaswa kuwa kiungo kinachowaunganisha Watanzania wote katika kujenga uchumi shirikishi.

Hali ya sasa ambapo itikadi za kisiasa zinatumiwa kama nyenzo ya kugawa wananchi inakwenda kinyume na maono ya Mwalimu, ambaye alikubali mfumo wa vyama vingi si kwa ajili ya kuleta utitiri wa makundi yanayohubiri utengano, bali kwa lengo la kuimarisha demokrasia kupitia itikadi mama ya taifa; Ujamaa na Kujitegemea.

Moja ya maeneo yaliyoguswa kwa uzito ni namna mfumo wa vyama vingi ulivyofifisha mifumo ya kiasili ya ulinzi na usalama, hususan uongozi wa nyumba kumi uliokuwa na uwezo wa kudhibiti uhalifu na matukio ya utekaji tangu ngazi ya chini kabisa.

Kwa sasa, viongozi wa ngazi hiyo wameanza kuonekana kama makada wa vyama badala ya kuwa walezi wa usalama wa jamii, jambo ambalo limeacha mwanya kwa wageni na watu wenye nia ovu kuingia mitaani bila kujulikana.

Kurudi kwenye misingi hiyo hakupaswi kutafsiriwa kama mkakati wa chama kimoja cha siasa, bali ni hitaji la kitaifa la kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao, huku miradi mikubwa ya kimkakati kama Reli ya Kisasa (SGR) ikitakiwa kutazamwa kama alama ya uunganisho inayowanufaisha wote bila kujali tofauti zao.

Wito umetolewa kwa Watanzania, hususan vijana wanaotumia mitandao kwa sasa, kuacha kufuata mkumbo wa mahubiri ya chuki na badala yake kuitumia teknolojia hiyo kueneza amani na uzalendo kama alivyofanya Mwalimu Nyerere katika kuipigania heshima ya Mwafrika.

Kujivunia nchi kunategemea uwezo wa kila mwananchi kuilinda misingi ya umoja iliyowekwa na wazee wetu, kwani bila mshikamano, Tanzania haiwezi kusimama na kujenga ustawi wa kudumu wa watu wake.

Ni wakati muafaka kwa kila mdau, kuanzia viongozi wa kidini hadi wa kisiasa, kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inatumika kama daraja la kuimarisha upendo na heshima miongoni mwa wananchi, huku wakikumbuka kuwa misingi hiyo hiyo ndiyo inayozisaidia nchi jirani kupiga hatua kubwa za mafanikio leo hii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com