
Wakati kukiwa na mfululizo wa mijadala na kelele kwenye mitandao ya kijamii inayojaribu kupotosha hali halisi ya nchi, takwimu za kimataifa zimeendelea kuumbua upotoshaji huo.
Taasisi ya Kimataifa ya Tathmini ya Uchumi, Fitch Ratings ya nchini Marekani, imetoa ripoti mpya inayothibitisha kuwa uchumi wa Tanzania uko kwenye mikono salama na unapaa kwa kasi ya kuridhisha.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Fitch imeipa Tanzania daraja la B+ lenye mwelekeo thabiti (Stable Outlook), ikibainisha kuwa jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua nchi na kupaisha uchumi zinaendelea kuzaa matunda ya kidhahiri.
Uchambuzi wa kiuchumi unaonesha kuwa, kinyume na upotoshaji unaoenezwa mitandaoni, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa takribani asilimia 6 ifikapo mwaka 2026 na 2027. Ukuaji huu unachagizwa na ufanisi katika sekta za kimkakati:Kilimo na madini ambapo kumekuwa na ongezeko la uzalishaji na mauzo nje ya nchi.
Aidha kukamilika kwa miradi ya kielelezo na kuanza kufanya kazi kwa baadhi yake kama Reli ya Kisasa (SGR) na mingine kukaribia kukamilika kama mradi wa Bomba la Mafuta la EACOP kutoka Hoima hadi Tanga kumetokea uhakika wa uelekeo wenye neema kuwa kwa Tanzania.
Ripoti hiyo ya Fitch inaenda sambamba na tathmini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwezi Februari 2026, inayothibitisha kuwa mfumuko wa bei nchini umebaki kuwa mdogo (ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5).
Hadi kufikia Januari 2026, mfumuko wa bei ulishuka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.6 ya Desemba 2025. Hii ni ishara tosha kuwa serikali imefanikiwa kulinda uwezo wa mwananchi wa kawaida kumudu gharama za maisha, licha ya changamoto za kiuchumi duniani.
Fitch imebainisha kuwa ushirikiano wa Tanzania na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) umeongeza imani ya wawekezaji wa nje. Aidha, ukusanyaji wa mapato ya kodi umeanza kuimarika, jambo linalopunguza nakisi ya bajeti na kusaidia kupunguza kasi ya ukuaji wa deni la taifa.
Wataalamu wa uchumi wanashauri kuwa, katika kipindi hiki ambacho takwimu za kimataifa zinaonesha mwelekeo chanya, ni muhimu kwa Watanzania kupuuza habari za upotoshaji zinazolenga kuleta taharuki.
Ingawa Fitch imetaja changamoto kama hitaji la kuongeza mapato ya ndani na kuimarisha taasisi, imesisitiza kuwa Tanzania iko kwenye "Mwelekeo Mzuri."
Social Plugin