
🟠Tume ya Madini yatangaza miradi, maeneo ya uchimbaji na mikopo ya uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027
📍Dodoma
Tume ya Madini imetangaza mipango ya miradi ya maendeleo na fursa mbalimbali kwa vijana katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Machi 16, 2026 kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema Tume imejipanga kutekeleza hatua mbalimbali zitakazoongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.
Amesema miongoni mwa mipango hiyo ni kuendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kupitia zabuni zitakazotangazwa, huku vijana wakihimizwa kufuatilia na kutumia fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Pia amesema Tume itaendelea kuandaa minada na maonesho ya madini ya vito pamoja na kutenga maeneo zaidi ya uchimbaji kwa vijana katika mikoa mbalimbali kulingana na aina ya madini yanayopatikana.
Aidha, Mhandisi Kamando amesema Tume ya Madini inaendelea kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia na kuwajengea vijana ujuzi wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika utafutaji na uchimbaji wa madini. Pia Tume inashirikiana na taasisi za kifedha ikiwemo benki ili kuweka utaratibu utakaowezesha vijana kupata mitaji ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Kuhusu utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Mhandisi Kamando amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 migodi ilinunua bidhaa na huduma kutoka kampuni za Watanzania zikiwemo zinazomilikiwa au kuajiri vijana zenye thamani ya shilingi trilioni 3.8, baada ya bidhaa na huduma 20 kutengwa mahsusi kwa kampuni zenye umiliki wa asilimia 100 ya Watanzania.
Pia amesema Tume ya Madini imeingia makubaliano na Benki ya CRDB yaliyosainiwa Februari 23, 2026 ili kuwasaidia wachimbaji wadogo wa dhahabu, hususan vijana, kupata mitaji ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Katika eneo la uongezaji thamani wa madini, Mhandisi Kamando amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kusimamia sera na sheria zinazohakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi. Hadi sasa kuna viwanda saba vya kusafisha madini vinavyofanya kazi nchini na sekta hiyo imezalisha ajira 273, nyingi zikinufaisha vijana, huku madini yenye thamani ya shilingi trilioni 5.802 yakiongezewa thamani ndani ya nchi kati ya Julai na Desemba 2025.
Aidha, amesema kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (Mining for Better Tomorrow – MBT), Tume ya Madini ilitoa leseni 273 kwa vikundi 183 vya vijana kati ya Julai na Desemba 2025 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mara, Kagera, Shinyanga, Morogoro, Dodoma na Njombe. Vikundi hivyo vinajihusisha na uchimbaji wa dhahabu, shaba, madini ya vito, chumvi na madini ya ujenzi, ambapo hadi Desemba 2025 vijana 2,550 walikuwa wamepata ajira za moja kwa moja kupitia mradi huo.
Pia amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo kwa kutoa leseni 5,983 kati ya Julai na Desemba 2025, sawa na asilimia 71 ya leseni zote zilizotolewa katika kipindi hicho.
Amebainisha kuwa leseni za uchimbaji mdogo hutolewa kwa Watanzania pekee, huku sehemu kubwa ya waombaji wakiwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45.
Kwa upande wa maeneo ya uchimbaji, Mhandisi Kamando amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imependekeza kutenga maeneo 65 maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika mikoa ikiwemo Mtwara, Manyara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Tabora, Geita, Shinyanga, Mwanza na Mbeya.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwapa fursa zaidi vijana kushiriki katika uchimbaji wa madini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.




Social Plugin